0
Mtu mwenye pumu huwa na mcharuko uvimbe sugu mwilini kwenye mirija yake ya kupitishia hewa (bronchioles tubes) hali ambayo husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hii na kuwa na ute mzito hivyo kupungua kwa njia ya kupitishia hewa.
Hali ambayo humfanya muathirika kushindwa kuvuta na kutoa hewa nje na hivyo kupumua kwa shida sana. Tatizo hili linaweza kudumu kwa muda mfupi au mrefu kiasi cha kuhitaji tiba ili kumuwezesha mgonjwa kupata nafuu.
Kutokana na kuwepo kwa msuguano na uzuiaji wa kupitisha hewa wakati wa kupumua hewa nje, pumu hujulikana pia kama obstructive lung disease .
Mtu aliye na pumu huwa na kipindi ambacho hawi na tatizo la pumu mpaka pale mwili unapochokozwa na kuingia katika hali hiyo. Wakati huo hote cha maisha yake kinachotokea ni kutulia tu mpaka pale inapotekea uchokozi mwilini.
Pumu inaweza kugawanywa katika makundi mawili, iko pumu ya ghafla ijulikanayo kitabibu kama Acute asthma. Wagonjwa wanaopatwa na kundi hili la pumu huwa na hali ya kawaida katika njia zao za hewa isiyobadilika wakati wa shambulio na usio wa shambulio.
Kundi nyingine ni Pumu sugu (Chronic Asthma). Kundi hili la pumu huwa na tabia ya kuwa na njia nyembamba za kupitisha hewa na kadiri jinsi mgonjwa anavyoendelea kupata matukio zaidi ya pumu njiaza hewa huzidi kuwa nyembamba na kusinyaa zaidi.
Aina za pumu
Bila kujalisha mgonjwa anaingia katika kundi gani, ugonjwa wa pumu unaweza kugawanywa katika aina kuu nne, ambazo ni inayobadilika, isiyobadilika, ya mazoezi na inayosababishwa na kazi.
Pumu inayobadilika (brittle asthma): Kulingana na tabia ya kujirudia rudia kwa matukio ya ugonjwa huu na madhara yake kwa mgonjwa, aina hii ya pumu inaweza kugawanywa zaidi katika aina nyingine mbili.
Aina ya kwanza ya pumu inayobadilika (type 1 brittle asthma) ni pumu yenye tabia ya kuwa na matukio na mashambulizi ya kubadilika kila mara japokuwa mgonjwa anaweza kuwa anapata matibabu kadhaa.
Aina ya pili ya pumu inayobadilika (type 2 brittle asthma) ni pumu ambayo mgonjwa anatokea kupata shambulizi la ghafla (asthmatic attack) wakati hapo awali ugonjwa wake uliweza kuthibitiwa kwa matibabu.
Pumu hatari isiyobadilika (status asthmaticus): Hii ni aina ya pumu iliyo hatari zaidi kwa mgonjwa. Pamoja na matumizi ya dawa kadhaa, zikiwemo vitanua njia za hewa (bronchodilators) na vipoza mcharuko mwili (steroids), mgonjwa wa aina hii ya pumu anaweza asipate nafuu ya haraka na anaweza kupoteza maisha.
Pumu inayosababishwa na mazoezi: Hali hii husababishwa na ufanyaji wa kupitiliza wa mazoezi ya viungo. Kwa kawaida wakati wa kufanya mazoezi mtu hupumua kwa kutumia pua na kupitia mdomo.
Hata hivyo, wakati mwingine hutokea hewa aivutayo huingia ndani ikiwa haijapozwa vya kutosha puani na hivyo kusababisha ongezeko la mtiririko wa damu katika mishipa inayosambaza damu katika mirija ya kupitisha hewa.
Hali hii husababisha kuvimba kwa kuta za mirija hiyo na muhusika kupata shambulizi la pumu. Aina hii ya pumu yaweza kudhibitiwa na dawa.
Inashauriwa sana kwa watu wenye matatizo kama haya kupasha moto misuli kwa mazoezi mepesi kabla ya kuanza mazoezi mazito na ya muda mrefu.
Pumu inayosababishwa na aina ya kazi: Mazingira ya kazi yanaweza kusababisha kutokea kwa pumu hata kwa baadhi ya wafanyakazi wasio na tatizo hili.
Aina hii huweza kuwatokea watu wanaofanya kazi kwenye viwanda vya kutengeneza matairi, vigae, rangi, kemikali mbalimbali, mbolea, chuma, unga, mbao na nguo.
Pumu husababishwa na nini?
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha kutokea kwa pumu au yanayohusishwa na shambulizi lake. Mambo hayo ni pamoja na matatizo ya vinasaba, maendeleo ya kiuchumi, magonjwa ya mapafu, moshi wa tumbaku, dawa za kushusha shinikizo la damu, uchafuzi wa mazingira, msongo wa mawazo na kichanga kuanza kutumia antibiotiki mapema.
Matatizo ya kinasaba yamehusishwa na kutokea kwa karibu asilimia 90 ya ugonjwa wa pumu hususani kipindi cha utoto.
Uvutaji wa sigara au tumbaku kipindi cha ujauzito pia unahusishwa na kusababisha pumu kwa mtoto atakayezaliwa.
Ugonjwa wa pumu umeonekana sana kwenye nchi zilizoendelea kiuchumi ikilinganishwa na nchi zenye maendeleo na hali duni ya kiuchumi. Sababu bado hazijawa wazi.
Magonjwa ya mapafu kama bronchitis, vyanzo vya mzio kama vile vumbi, vinyesi vya wanyama na baadhi ya vyakula, vinaweza kuchoche tatizo hilo.
Uchafuzi wa mazingira kama moshi na baadhi ya harufu kali, Baadhi ya kemikali kwenye maeneo ya kazi hasa kwenye viwanda kama vya rangi, chuma, sementi na vigae.
Baadhi ya wagonjwa wanaotumia dawa za kushusha shinikizo la damu zilizo katika jamii ya beta-blockers kama vile propanolol wapo katika hatari ya kupata shambulio la ugonjwa wa pumu.
Magonjwa kwenye mfumo wa kupumua yasabishwayo na baadhi ya virusi na bakteria kama vile rhinovirus, Chlamydia pneumonia au Bordetella pertusis.
Matumizi ya mapema sana ya baadhi ya dawa hasa antibiotiki kwa watoto yanaweza kubadilisha mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya magonjwa na hivyo kumfanya mtoto kuwa katika hatari ya kupata pumu.
Ongezeko la msongo wa mawazo huweza kusababisha pumu na matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Upasuaji wakati wa kujifungua (caesarian section), Tafiti kadhaa zimeonyesha kuwa kujifungua kwa njia ya upasuaji huongeza uwezekano wa kupata pumu kwa vile njia hiyo yaweza kuathiri mfumo wa kinga ya mwili dhidi ya maradhi.
Vihatarishi vya ugonjwa wa pumu
Uwezekano wa kupata ugonjwa wa pumu huongezeka iwapo mtu atakuwa na magonjwa ya mzio kama vile magonjwa ya ngozi (eczema) au homa isababishwayo na aina fulani ya vumbi, vumbi la maua au chavua, matumizi ya asprini na maambukizi ya ugonjwa wa virusi.
Vile vile kama anaishi sehemu zenye baridi au hewa yenye unyevu na vumbi, matatizo katika njia yake ya chakula ikiwamo uchokozi wa kujaa tindikali na gesi tumboni.
Dalili za ugonjwa wa pumu
Dalili za ugonjwa wa pumu ni pamoja na kuishiwa na pumzi, kupumua kwa shida huku pumzi zikikata, kutoa sauti kama mtu anayepiga miluzi wakati wa kupumua (wheezing), kukohoa sana hasa nyakati za usiku au asubuhi. Kikohozi huambatana na kutoa makohozi mazito, yasiyo na rangi au yenye rangi ya njano.
Kubana kwa kifua kwa mtu aliyepata shambulizi kubwa la pumu na atashindwa kuzungumza na pia kuwa na hali kama ya kuchanganyikiwa huku.
Matibabu ya Pumu
Kwa ujumla matibabu ya pumu hujumuisha kuepuka visababishi/ vianzisha mzio vya ugonjwa huu na matumizi ya madawa kwa walio na hali mbaya.
Kwa wagojwa wanaopata ugonjwa huu kwa sababu ya msongo wa mawazo hupewa ushauri nasaha kwa ajili ya kusaidia kutatua matatizo yanayowakabili.
Vilevile inashauriwa kwa wenye tatizo hili kuwa na dawa karibu muda wote kwa ajili ya matumizi pindi shambulizi litakapotokea. Vilevile inashauriwa kuepuka mazingira na hali za baridi ambazo huweza kuchochea kutokea kwa shambulio la ugonjwa huu.
Matibabu ya kutumia dawa hujumuisha matumizi ya dawa za kusaidia kupunguza na kuondoa makohozi (expectorants) na dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa (bronchodilators).
Zipo dawa pia pia za kuondoa mcharuko mwili na zile za kuzuia mzio Hata hivyo, kuna matibabu ya ziada kulingana na hali ya mgonjwa pamoja na kundi na aina ya pumu inayomuathiri.
Kwa wagonjwa wenye pumu ya ghafla na wenye hali mbaya matibabu hujumuisha matumizi ya dawa za kutanua mirija ya hewa, (bronchodilators) pamoja na kuongezewa hewa ya oksijeni.
Vilevile dawa za kutuliza mcharuko mwili (steroids) pamoja na dawa za kutuliza kukakamaa kwa misuli ya mwili (intravenous muscle relaxants). Kwa wagonjwa wenye pumu sugu, jambo la muhimu ni kuepuka visababishi na matumizi ya dawa zinazosaidia kutanua mirija ya hewa.
Ni vema pia kuepuka matumizi ya dawa za jamii ya beta-blockers kwa wagonjwa wenye shinikizo la damu na ambao pia wana pumu. Dawa hizi huleta uchokozi na mgonjwa hupata kikohozi na kubanwa.

Post a Comment Blogger

 
Top