0
JESHI la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia mkazi wa Katesh katika wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Mohammed Abdallah (35), baada ya kukutwa akitoa huduma za kidaktari ambazo hana utaalamu wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema Abdallah alikamatwa Agosti 12, mwaka huu saa tisa mchana katika kijiji cha Nyerere kata ya Hogoro tarafa ya Zoissa wilaya ya Kongwa, akiwa tayari ametoa huduma ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 20.

Kabla ya kukamatwa kwake, Kamanda Misime alisema Polisi ilipata taarifa za siri na kuzifanyia kazi, ambapo mtuhumiwa alikamatwa katika nyumba isiyostahili kufanyiwa shughuli za matibabu mali ya Sikitu Magomba.

Kamanda Misime alisema baada ya mtuhumiwa kukamatwa katika nyumba hiyo alikopanga, alipopekuliwa, alikutwa na dawa mbalimbali zenye nembo ya Bohari ya Madawa (MSD), mifuko tisa ya dripu za ujazo wa milimita 500, ambazo kwa kawaida haziruhusiwi kuuzwa, sindano na baadhi ya vifaa tiba vinavyodhaniwa vilipatikana kwa njia isiyo halali.

Baada ya kuhojiwa, kwa mujibu wa Kamanda Misime, mtuhumiwa alikiri kutenda kosa hilo na kuongeza kwamba hana taaluma yoyote ya utabibu na elimu yake ni darasa la saba. Kamanda Misime alisema uchunguzi zaidi unaendelea na ukikamilika, mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.

Alitoa mwito kwa wananchi kuwa makini na kuhakikisha wanatibiwa kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zinazofahamika, ili kuepuka madhara dhidi ya tiba bandia.
 
Pia alitaka wananchi kufichua madaktari feki, ili wachukuliwe hatua za kisheria, kwani wanapotibiwa na mtu ambaye hana utaalamu, kwanza huwatapona na pili watapata madhara ambayo yanaweza kuwa ya kudumu na pengine kupoteza maisha

Post a Comment Blogger

 
Top