WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) imepiga marufuku usafirishaji wa mazao ya misitu ikiwemo mkaa ambapo mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo ambavyo Serikali inavihitaji, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo wake.
Imesema zuio hilo linakwenda sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo ya miti kwenda nje ya nchi, magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa, pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda sehemu moja hadi nyingine mijini na vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisema uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya maduhuli stahiki ya rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.
Alisema moja ya majukumu ya TFS, ni kuhakikisha inaanzisha na kusimamia rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni kosa kuvuna hovyo misitu na bidhaa zake bila kibali.
Mtendaji huyo alisema kila zao linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru stahiki na kukatiwa risiti, hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia mbalimbali zinazokatazwa ni kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.
“Mazao ya misitu, ikiwemo mikaa ni kosa kuuzwa na kusafirishwa bila kuwepo kibali na risiti. Muuza mkaa lazima uwe na risiti, na wewe mnunuzi tukikukamata na gunia la mkaa na huna risiti utawajibika.
“Tunataka kuhakikisha maduhuli ya mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata matumizi endelevu ya rasilimali za misitu hivyo ni biashara hii ya miti, mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe wazi.
“Ni marufuku kusafirisha mazao ya misitu usiku, kama mtu ana vigezo vyote tunavyovihitaji kusafirisha mazao ya misitu anatakiwa kusafiri kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni, ikipita hapo, weka pembeni gari mpaka asubuhi,” alisema.
Aidha alisema TFS chini ya Wizara ya Maliasili ina Meneja miti kwenye kila wilaya, ambao wanafanya kazi kwa karibu na Maofisa Watendaji wa vijiji ambao hushirikiana kutoa vibali kwa kuvuna miti stahiki kisheria na kutoa risiti.
Alisema risiti hizo pamoja na vigezo vingine ikiwemo kuwa na usajili wa TFS, leseni ya biashara na namba ya utambulisho wa mfanyabiashara (TIN), hati ya kusafirisha mazao ya misitu humfanya mfanyabiashara kuruhusiwa kuendelea na biashara ya mazao ya miti nchini.
Profesa Silayo alisema TFS wataendelea na majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozungumza na watumishi wa wizara hiyo mapema mwezi uliopita.
Baadhi ya maagizo hayo likiwemo la kupunguza vizuio kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, Silayo alisema wanafanya utafiti kujua kizuizi gani kitolewe na kipi kibaki sambamba na kubana uvunaji holela wa misitu.
Alisema lengo lao si kukamata magogo baada ya kuvunwa bali ni kuzuia misitu isiharibiwe hivyo inapotokea, hutumia vizuio hivyo kukagua na kukamata nyara hizo za serikali ili kuongeza maduhuli kwa mujibu wa sheria.
“Tumeanza kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu, ambayo kiuhalisia yana ukweli mkubwa kwa hiyo tunataka kuondoa vizuizi visivyo na tija lakini pia kuwasisitizia watu wetu kule vituoni kuzingatia weledi.
“Tayari tumeanza kutumia mashine za kielektroniki za malipo yaani EFD kwenye vizuio vyetu mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro na tutaendelea kuzisambaza maeneo mengine mara tu TRA watakapoziingizia program yao ya malipo,” alisema.
Alisema wana changamoto kadhaa ikiwemo uhaba wa vitendea kazi hususan magari lakini wanafanya jitihada mbalimbali kuhakjikisha wanazitatua ili misitu iwe na mchango kwenye pato la taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo, alisema kitakwimu asilimia 94 za kaya zote takriban milioni tisa nchini zinatumia mkaa kama nishani kuu, huku maeneo ya mijini pekee ikiwa na asilimia 38 za watumia mkaa.
“Mahitaji ya miti ni mita za ujazo 62.3 huku uwezo ukiwa ni mita za ujazo 42.8 hivyo uharibifu wa misitu unafika hekta 372,000 kwa mwaka sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti,” alisema Kilongo.
Alisema kwa takwimu hizo, miti na misitu nchini imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa na kusababisha uhitaji wa hekta mpya 185,000 za misitu inayotakiwa kupandwa maeneo mbalimbali ya nchi.
“Upungufu huu ni kichocheo cha uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata ndani ya hifadhi za taifa hivyo suala la kuilinda ni jukumu letu sote, kila gunia lazima lilipiwe ushuru,” alisema.
Pia alisema katika jitihada za kurudisha misitu iliyopotea, upo mkakati wa kitaifa wa kupanda miti ambapo kwa kila wilaya imepewa jukumu la kupanda miti milioni moja na nusu kwa mwaka chini ya uangalizi wa Meneja misitu wa wilaya husika.
Wiki kadhaa zilizopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Dar es Salaam, alisema nchi inageuka jangwa kutokana na misitu mingi kukatwa kiholela huku maduhuli ya serikali yakipotea.
Kauli hiyo inaonekana kuanza kuzaa matunda baada ya TFS kuamua kuongeza kasi ya usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki nchini kwa siku za hivi karibuni hatua ambayo inadaiwa kuwa endelevu.
Post a Comment Blogger Facebook