0
Dar es Salaam. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mechi ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Kagame kati ya Yanga na Gor Mahia.
Dk Magufuli aliyepitishwa na mkutano mkuu wa chama hicho, Jumatatu mjini Dodoma amepewa heshima hiyo ikiwa ni kutambua mchango wake katika maendeleo wakati akiwa waziri.
Hilo litakuwa kusanyiko la kwanza kwa mwanasiasa huyo ambaye hakuwahi kujiainisha kwenye ushabiki wa soka, hasa kwa klabu kubwa, Simba na Yanga.
Wakati hayo yakiendelea, Shirikisho la Soka Tanzamia (TFF) limeahidi kuweka ulinzi maalumu wakati wa mashindano hayo.
Shirikisho hilo limeahidi usalama na ulinzi wakati wakati wote mashindano hayo kwa mashabiki na timu zote zitakazoshiriki.
Hakikisho hilo la TFF limekuja siku chache kufuatia kuibuka kwa matukio ya uhalifu jijini Dar es Salaam yanayohusisha uvamizi wa vituo vya polisi kwenye maeneo kadhaa.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na TFF ni kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vimeombwa kutoa ulinzi maalumu kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.
Ulinzi huo kwa timu utahusisha misafara, hoteli zote ambako timu hizo zitafikia huku mikakati kiulinzi, ikiwa pia kwa mashabiki kwenye viwanja vitakavyotumika, Karume na Taifa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa pamoja na vyombo vyote vya ulinzi na usalama, pia wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha hakuna matukio ya aina yoyote yanayoweza kuvuruga au kuhatarisha amani kipindi chote cha michezo hiyo.
“Tunawahakikishia wapenzi wa soka na Watanzania kwa jumla kuwa kutakuwa na usalama wa kutosha kwani vyombo husika tayari vimeshachukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa hakuna aina yoyote ya uvunjifu wa amani na ulinzi utakuwa ni wa uhakika, hivyo mashabiki wasiwe na wasiwasi,” alisema Kizuguto.
Katika hatua nyingine, Alhamisi kutakuwa na mtihani maalumu kwa waamuzi, Cooper Test ambako wale wakatakaofuzu ndiyo watachezesha mashindano hayo

Post a Comment Blogger

 
Top