0

Dar es Salaam. Wakati mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM ukiwa umekamilika, ni dhahiri kwamba baadhi ya vigogo waliokuwa na matumaini makubwa ya kuukwaa, sasa wanaugulia maumivu huku wengine wakiwa wameshautangazia umma kutoendelea na ubunge.
Licha ya kuwa siasa ni pata potea, kwa wanasiasa vijana huenda mchakato huo ukawa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio na kwa baadhi ya vigogo huenda ukawa ndiyo mwanzo wa kuelekea kustaafu siasa.
Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Dk Mohammed Gharib Bilal, Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Samuel Sitta na Profesa Mark Mwandosya ni makada waliojitokeza kujaribu bahati yao ya kuteuliwa kugombea urais, lakini ni dhahiri kuwa sasa watakuwa wanaanza kujiwekea mazingira ya kuachana na siasa.
Wote hawakumudu kuingia kwenye orodha ya wagombea watano waliopelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchujwa hadi kubakia watatu ambao hupelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kumpata mgombea urais wa CCM.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM wa kumuachia mteule agombee kwa vipindi viwili iwapo anashinda uchaguzi wa Rais, makada hao sasa watalazimika kusubiri hadi mwaka 2025 ili kujaribu tena bahati yao, jambo ambalo linaonekana halitakuwa rahisi.
“Nyakati za kisiasa zinabadilika haraka sana. Miaka 10 ijayo siyo mchezo,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Hamad Salim alipohojiwa na Mwananchi kuhusu mustakabali wa makada waliokosa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Kwa kipindi hicho, mambo mengi yatabadilika, wanasiasa waliogombea kipindi hiki hawawezi kuwa kwenye umaarufu wa sasa, wanaweza kupanda chati au kushuka.
 “Pia, kuna suala la umri wazee kama Dk Bilal au Sumaye miaka 10 ijayo kupanda jukwaani na kushuka mara kwa mara itakuwa shida kidogo. Wanasiasa wengi waliokuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho ni wazee na ule siyo umri wa kushinda majukwaani.”
Licha ya sifa za mgombea kutozungumzia umri wa juu bali wa chini ambao ni kuanzia miaka 40, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alishauri baadhi ya vigogo walioshindwa kupumzika kupisha damu changa za mabadiliko.
Alisema: “Siasa nchini hazitabiriki na ni za kipekee kwani unaweza ukawa maarufu usichagulike na siku zinavyokwenda ukapoteza umaarufu huo.
“Kwa hali ya sasa, Bilal, Pinda, Lowassa, Sitta tayari walishakamata nafasi za juu nchini na umri wao umeshasogea. Bila shaka ni muda muafaka kupisha wengine… wameshaitumikia nchi vya kutosha na wana marupurupu ya kutosha baada ya kustaafu. Ni bora wawaachie vijana walete mabadiliko,” alisema Mbunda.
Alisema makada hao ni washauri wazuri iwapo wataachana na siasa za kushindana. Alisema hata kwa wale ambao umri unawaruhusu, haitakuwa vizuri kuwapa vyeo vidogo kama vya ubalozi na kwa maana hiyo alisema safari yao kisiasa, imefikia ukingoni.

Post a Comment Blogger

 
Top