0
Mshambuliaji Malimi Busungu (kulia) akipongezwa
Dar es Salaam. Pamoja na kupata ushindi wa mabao 3-0 jana, Yanga iliweka rekodi mbaya ya kukosa penalti mbili ndani ya dakika 10 za mchezo huo dhidi ya Djibouti Telecom kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo, mshambuliaji Malimi Busungu aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo na kuzawadiwa king’amuzi aliiokoa timu yake baada ya kuifungia mabao mabao mawili, dakika ya 26, akiunganisha krosi ya beki Mghana Joseph Zuttah na kuongeza la pili dakika 65, akiunganisha krosi ya kinda aliyeng’ara Geofrey Mwashiuya.
Chipukizi huyo aliyeingia uwanjani kipindi cha pili akitokea benchi alifunga bao la tatu kwa juhudi binafsi baada ya kuwatoka mabeki wa Telecom na kupiga shuti lililogonga mwamba, kisha kumgonga mgongoni kipa Nzokira Jeef na kuingia wavuni na kuiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa robo fainali ya mashindano ya Kombe la Kagame.
Yanga iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 2-1 na Gor Mahia ya Kenya Jumamosi kwenye mechi ya ufunguzi pamoja na kukosa penalti iliyopigwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kadi nyekundu ya mshambuliaji wake, Donald Ngoma.
Jinamizi la kukosa penalti liliendelea kuiandama timu hiyo baada ya washambuliaji wake vinara wa ufungaji msimu uliopita, Amissi Tambwe na Simon Msuva kukosa penalti ndani ya dakika 10, huku Cannavaro akijiweka kando wakati wa upigaji wa penalti hizo.
Tambwe alikosa penalti yake dakika 39, baada ya Msuva kuangushwa ndani ya eneo la 18 na beki wa Telecom, Warsama Ibrahim aliyepewa kadi ya njano kwa kitendo hicho.
Wakati mashabiki wakishangaa, Tambwe kukosa penalti hiyo katika dakika 45, Yanga ilipata penalti ya pili iliyopigwa na Msuva iliyoshia mikononi mwa kipa wa Telecom, Jeef na kuwafanya mabingwa hao mara tano wa Kagame kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kutokana na kukosa penalti hizo, kocha Hans Pluijm aliwapumzisha Msuva na Tambwe na kuwaingiza Mwashiuya na Kpah Sherman wakati Telecom ilimtoa Said Elmi na kumwingiza Warsama Said.
Kipindi cha pili Telecom iliyovaa jezi nyekundu na kushangiliwa kwa nguvu na mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Simba ilianza kucheza kwa kujiamini kulinganisha na dakika 45 za kwanza ambacho Yanga ilitegeneza nafasi nyingi, lakini washambuliaji wake walikosa umakini.
Yanga iliyocheza mfumo wa 4-3-3, ilitawala vizuri katikati ya uwanja baada ya kuingia kwa Mwashiuya na Sherman waliokuwa na maelewano mazuri na viungo wa Salum Telela, Deus Kaseke.
Kwa matokeo hayo, Yanga inahitaji ushindi dhidi ya KMKM ya Zanzibar ili kujihakikishia kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Katika mchezo wa mapema, wawakilishi wa Zanzibar, KMKM walijiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwa robo fainali baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Al- Kahrtoum ya Sudan kwenye uwanja huo.
Mshambuliaji Salah Bilal alifungia Al- Khartoum bao la kuongoza, dakika ya 7, likiwa ni bao lake la tatu katika mashindano hayo ya mwaka huu na kumfikia kiungo mshambuliaji wa Gor Mahia, Michael Olunga mwenye idadi hiyo.
KMKM ilisawazisha bao hilo kipindi cha pili kupitia kwa Simon Mateo dakika ya 58, akitumia mpira mrefu uliopigwa na kipa wake ulioshindwa kuolewa na mabeki wa Al Khartoum uliompa mwanya mfungaji kufunga bao hilo ambalo ni la pili kwake.
Al- Khrtoum iljihakikishia pointi tatu muhimu na nafasi kwenye robo fainali baada ya kupata bao la pili, dakika 84, lililofungwa na Anthony Agay.
Katika mchezo wa Kundi C, uliochezwa Uwanja wa Karume, KCCA ya Ugand imeziduka kwa kuichapa Adama City ya Ethiopia kwa bao 1-0.

Post a Comment Blogger

 
Top