0
MPENZI msomaji wa ukurasa huu wa afya, leo tuangalie ugonjwa unaojulikana kama mkanda wa jeshi. Tumekuwa tukishuhudia baadhi ya watu wenye ugonjwa huu wakionekana kuwa wana maambukizi ya VVU bila kuwa na uhakika wa afya zao au bila kutambua chanzo sahihi cha ugonjwa wenyewe.

Hali hii imewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa mtu mwenye ugonjwa wa mkanda wa jeshi anakuwa na ugonjwa wa UKIMWI  jambo ambalo halina ukweli kwa asilimia mia moja kwani sio wote wenye ugonjwa huu wanakuwa na VVU.

Ugonjwa huu kitaalamu unajulikana shingles au herpes zoster ambapo ugonjwa huu husababishwa  na virusi aina ya Varicella-zoster ambao pia husababisha ugonjwa wa tetekuwanga. Ugonjwa huu wa mkanda wa jeshi huathiri ngozi ambapo huambatana na vipele na michubuko kama ya  kuungua yenye kuambatana na maumivu makali.

Visababishi
Dk Grace Chirwa kutoka Hospitali ya Temeke Dar es Salaam anasema kuwa ugonjwa huu husababishwa na virusi aina ya Varicella-zoster  ambao pia husababisha ugonjwa wa tetekuwanga. Baada ya mtu kupatwa na ugonjwa wa tetekuwanga, virusi vya ugonjwa huo hubaki katika hali ya kupooza/ kutokuwa na madhara katika baadhi ya neva mwilini.

Baada ya kukaa mwilini kwa miaka kadhaa, iwapo kinga za mwili zitashuka kwa sababu yoyote virusi hawa hupata nguvu na kuwa imara jambo linalopelekea kutokea kwa ugonjwa wa mkanda wa jeshi. Ugonjwa huu unapotokea ni mara chache sana ugonjwa huo kujirudia mara ya pili kwa maisha ya mtu huyo.

Vihatarishi
Ugonjwa huu unaweza kumpata mtu wa umri wowote ingawa watu wa makundi fulani wanakuwa katika hali ya hatari zaidi kupatwa na ugonjwa huo.
Makundi ambayo yapo kwenye hatari zaidi ni watu walio na umri wa zaidi ya miaka 60, mtu aliyewahi kuugua ugonjwa wa tetekuwanga kabla ya kufikisha umri wa mwaka mmoja.
Pia watu ambao kinga zao za mwili zimepungua kwa sababu zozote zile ikiwemo mwenye maambukizi ya HIV, saratani pamoja na utapiamlo:

Licha ya hiyo ugonjwa huu hauambukizwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kama yalivyo magonjwa mengine. Inapotokea mtoto au mtu mzima ambaye hajawahi kupata ugonjwa wa tete kuwanga au kupata chanjo yake akakutana na mgonjwa wa mkanda wa jeshi, mtoto huyo au mtu huyo anaweza kuugua ugonjwa wa tetekuwanga na siyo mkanda wa jeshi.

Dalili
Dk Chirwa anasema kuwa dalili ya awali kabisa ya mkanda wa jeshi ni maumivu makali sehemu fulani/ upande mmoja wa mwili yanayoambatana na hali ya ganzi na hisia za kuungua kwenye ngozi.
Maumivu hayo pamoja na   hisia hizo za kuungua  hutokea kabla ya vipele/ michubuko kutokea kwenye ngozi.

Kawaida ya dalili hizi za vipele au michubuko huusisha eneo fulani la mwili hasa kuanzia kwenye uti wa mgongo kuzunguka kuelekea eneo la tumbo au kifua. Michubuko pia inaweza kutokea kwenye maeneo yanayozunguka uso, macho, midomo au masikio.
Dalili nyingine za ugonjwa huu ni maumivu ya tumbo, homa, maumivu ya mwili mzima, kuwa na vidonda sehemu za siri, kuwa na maumivu katika sehemu za kichwa, kuwa na maumivu ya viungo, kuvimba kwa tezi pamoja na tatizo la kutoona iwapo  neva za maeneo ya uso zimeathirika.

Vipimo
Ni mara chache sana kufanya vipimo kwa ajili ya kutambua ugonjwa huu, isipokuwa kwa nchi zilizoendelea. Kwa ujumla utambuzi wa ugonjwa huu hufanyika kwa kuangalia historia ya mgonjwa na kuchunguza sehemu ya ngozi iliyoathiriwa. Pia vipimo vya damu FBP huonesha ongezeko la chembe nyeupe za damu.

Matibabu
Matibabu ya mkanda wa jeshi hujumuisha matumizi ya dawa kama vile Acyclovir, Famciclovir na Valacyclovir kwa ajili ya kuua virusi wanaosababisha ugonwja huu. Dawa hizi husaidia kupunguza maumivu, kuzuia madhara zaidi ya ugonjwa huu na kupunguza muda wa ugonjwa.
Dawa hizi hutolewa angalau saa 72 baada ya mgonjwa kuanza kuhisi maumivu na hali ya kuungua.Wataalamu wa afya hushauri mgonjwa kuanza kutumia dawa kabla  vipele/ michubuko kujitokeza.

Jamii ya dawa za corticosteroids kama vile prednisolone husaidia kupunguza maumivu na uvimbe kwa badhi ya wagonjwa. Dawa nyingine zinazofaa kutumika ni pamoja na jamii ya antihistamines kwa ajili ya kupunguza muwasho, dawa za maumivu, calamine lotion kwa ajili ya kupunguza muwasho. Aidha mgonjwa anashauriwa kupata mapumziko ya kutosha

Matarajio
Ugonjwa huu huchukua kati ya wiki mbili hadi tatu kupona wenyewe, na unapo pona inakuwa nadra sana mtu aliyewahi kuugua kurudiwa tena na ugonjwa huu kwa mara ya pili. Licha ya kupona kwa kipindi hicho, uwezekano wa maumivu yanayotokana na ugonjwa huo kudumu kwa muda wa miezi kadhaa hadi kwa mmoja unakuwepo ambapo husababishwa na uharibifu katika neva za mwili.

Madhara
Mtu aliyeugua ugonjwa huu anakuwa katika hatari ya kupatwa na  a kupatwa na shambulio jingine la ugonjwa huu, maambukizi ya bakteria, upofu iwapo eneo la jicho litahusika, ukiziwi, maambukizi katika utando wa ubongo (encephalitis), uwepo wa vimelea kwenye damu (sepsis) au ugonjwa unaoitwa Ramsay Hunt Syndrome iwapo utahusisha neva za uso.

Kinga
Ni muhimu sana watu kuepuka kugusa eneo lenye vipele au michubuko kwa mtu mwenye mkanda wa jeshi au tetekuwanga iwapo mtu anayetaka kufanya hivyo hajawahi  au kupata chanjo ya tetekuwanga.
Ni vema kupata chanjo dhidi ya virus wa Varicella zoster kama inapatikana katika nchi au eneo ulilopo ili kuepukana na kupatwa na tetekuwanga au mkanda wa jeshi.

Post a Comment Blogger

 
Top