0
wapenzi na karibuni katika kipindi kingine cha Ijue Afya Yako. Kipindi ambacho hujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu afya na tiba yakiwemo magonjwa na namna ya kujikinga nayo ili kuiwezesha jamii kuimarisha afya kwa ujumla. Katika kipindi chetu cha leo na vinavyofuata tutazungumzia matatizo ya figo na kile kinachosababisha viungo hivyo muhimu mwilini vishindwe kufanya kazi. Tumeamua kuzungumzia maudhui hiyo kutokana na watu wengi katika jamii yetu kukabiliwa na matatizo tofauti ya figo ambayo matibabu yake ni yenye gharama kubwa na ambayo pia husababisha baadhi kupoteza maisha.

Hapa duniani kuna maradhi ya aina nyingi yanayotisha, kusumbua binadamu, kuwatia ulemavu na hata kuwa chanzo cha uchumi kutetereka na wakati mwingine kusababisha vifo. Miongoni mwa maradhi hayo ni kuharibika kwa figo au kushindwa kufanya kazi. Ugonjwa huo si tu kwamba huleta maumivu kwa mgonjwa, bali pia hautibiki kirahisi pamoja na gharama za matibabu husika kuwa kubwa huku wengi wakishindwa kuzimudu. Wataalamu wa afya wanasema kuwa, kuna sababu kadhaa zinazosababisha maradhi ya figo yakiwamo matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, dawa za kienyeji, uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupita kiasi. Lakini kabla hatujaeleza jinsi tatizo hilo linavyotokea kwanza tufahamu figo ni nini na ni zipi kazi zake.

Figo ni miongoni mwa viungo muhimu katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu, vyenye kazi ya kuchuja uchafu uliomo kwenye damu. Mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana ambazo ziko kila upande wa uti wa mgongo, na zimejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu. Figo hukaa karibu na tumbo mbele ya ukuta wa mgongo. Hupata damu kutoka kwenye mishipa ya ateri moja kwa moja kutoka kwenye mshipa mkuu wa aota na kuirudisha damu hiyo moja kwa moja kwa mishipa ya veini kwenda kwenye vena cava.

Figo huhusika na uratibu wa shinikizo la damu, madini ndani ya damu na uzalishaji wa chembe nyekundu za damu. Lakini kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu katika damu, kusaidia kuhifadhi na kudhibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Figo pia huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku zikinyonya madini na kemikali muhimu na kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika. Kazi nyingine za figo ni pamoja na kusaidia kutengeneza mada ya erythropoletin ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, hupokea asilimia 25 ya damu na kila figo ina chembechembe hai ndogo milioni moja, ambapo pia husaidia kudhibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure).

Jinsi figo zinavyofanya kazi
Figo zina jukumu kubwa katika mwili, sio tu kuchuja uchafu kwenye damu ili kuepukana nao, bali kuratibu madini yaliyomo ndani ya damu, shinikizo la damu na kuchochea uzalishaji wa chembechembe nyekundu za damu. Figo zina uwezo wa kufuatilia kiwango cha umajimaji wa damu na uongezekaji wa madini kama vile sodiamu na potasiamu na pia tindikali katika mwili mzima. Huchuja uchafu wa vyakula vilivyosharabiwa mwilini. Uchafu mkubwa unaochujwa mwilini ni pamoja na urea ya nitrojeni (blood urea nitrogen-BUN) na creatinine (Cr). Damu inaposhuka kwenye figo, vichocheo vyake huamua kiasi gani cha maji kiende kuwa mkojo kulingana na wingi wa madini yaliyomo ndani ya damu. Kwa mfano, kama mtu anaharisha au ameishiwa na maji kutokana na ugonjwa fulani, figo huzuia maji yaliyopo yasiende kuwa mkojo na hapo mkojo huwa wa njano.

Lakini kama maji yako mengi mwilini, mkojo huwa na maji na huonekana msafi. Kazi hiyo hufanywa na homoni inayoitwa renin ambayo huzalishwa na figo ikiwa ni sehemu ya uratibu wa shinikizo la damu na hali ya mwili.

Figo pia huzalisha homoni ya 'erythropoietin' ambayo huchochea uti wa mgongo kuzalisha chembechembe nyekundu za damu. Kuna seli maalumu katika figo ambazo huratibu kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya damu. Kama kiwango hicho kitashuka 'erythropoietin' huongezeka na kuchochea uzalishaji wa chembe nyekundu za damu. Baada ya figo kuchuja uchafu, mkojo huzalishwa na kupelekwa kwenye kibofu kupitia mrija wa ureta ambako huhifadhiwa hapo ukisubiri kutoka nje ya mwili kwa kukojoa.

Kati ya sababu nyingi zinazopelekea figo kushindwa kufanya kazi ni shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari. Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya watu wazima wenye matatizo ya figo husababishwa na magonjwa hayo. Ugonjwa wa kisukari kama haujatibiwa ipasavyo, sukari itajilimbikiza ndani ya damu na ikiwa nyingi huharibu seli na hivyo kupunguza uwezo wa figo kuchuja uchafu. Kuna aina mbili za kisukari, kwanza ni kisukari ambacho mwili hushindwa kuzalisha mada inayomeng'enya sukari kwenye damu yaani insulin, na kisukari cha pili ni pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri insulin inayozalishwa. Kuhusiana na tatizo la shinikizo la juu la damu, ni pale kunapokuwa na shinikizo kubwa la damu kuliko ukubwa wa mishipa yake. Shinikizo hilo linapoongezeka husababisha ugonjwa wa moyo na pia ugonjwa sugu wa figo.

Sababu nyingine ni kuharibika kwa seli zinazohusika na uchujaji wa uchafu hali inayosababisha kupungua kwa mkojo, kutotolewa kwa protini katika mkojo na kuvimba kwa mikono na miguu. Sababu nyingine ya kuharibika figo ni magonjwa ya kurithi kama vile 'Polycystic' yaani kutokea vivimbe ndani ya figo na hivyo kushindwa viungo hivyo kufanya kazi. Magonjwa kama haya siyo ya kawaida lakini huanza wakati mtoto akiwa bado tumboni. Aina za ugonjwa wa figo
Aina za ugonjwa huu ni mbili, ya kwanza ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi, na ya pili ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.

Katika aina hii ya ugonjwa ambapo figo hushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu, kiungo hicho huharibiwa taratibu na kuendelea kupungua uwezo wake wa kufanya kazi kadiri siku zinavyokwenda. Dalili za aina hii ya ugonjwa huchelewa kujitokeza na wakati mwingine mwenye tatizo huwa hahisi dalili yeyote, hadi pale inapotokea akaugua ugonjwa mwingine na daktari kuhisi tatizo, ndipo hugundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya vipimo.

Sababu zinazotajwa kupelekea figo kushindwa kufanya kazi ghafla, kubwa ni kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye figo, kemikali za mwilini au kushambuliwa na sumu. Kushuka kiwango cha mzunguko wa damu humpata mtu ambaye anatapika sana na hanywi maji ya kutosha, anayeharisha sana na hanywi maji ya kutosha na wale ambao hupoteza damu nyingi kama vile kwenye ajali. Sababu nyingine ni pamoja na ugonjwa wa moyo, ambapo moyo kushindwa kusukuma damu kwa ghafla, au waliougua maradhi ya moyo kwa muda mrefu.

Kemikali pia husababisha hali hiyo ambayo hutokana na kutumia dawa iliyo na mzio kwa mtumiaji, dawa zinazosababisha mkojo utoke kwa wingi, dawa za kienyeji na baadhi ya dawa za malaria. Tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla pia humpata mtu ambaye ana bakteria kwenye mzunguko wa damu, ambao wanaweza kusababisha homa yaani Septicemia na hata kuugua malaria. Lakini sababu zinazofanya figo zishindwe kufanya kazi taratibu na kwa muda mrefu na hatimaye kuharibika kabisa, ni presha kuwa juu, kisukari, magonjwa yanayosababishwa na bakteria, virusi vya HIV, saratani na sumu mbalimbali zinazoingia mwilini.

Dalili
Dalili za kushindwa kufanya kazi figo ni pamoja na kuongezeka kwa uchafu ndani ya mwili ambao husababisha kwanza kabisa kupungua kwa kiasi cha mkojo, kushindwa kupumua, kusikia kichefuchefu, kutapika na kuvimba miguu. Dalili nyingine ni maji kujaa mwilini, madini ya mwili kuwa juu hasa ya 'potashiamu', asidi nyingi, matatizo katika moyo, ubongo, kukosa hamu ya kula na kudhoofika mwili.

Hali hiyo husababisha udhaifu, kuhema kwa shida, uchovu na kuchanganyikiwa. Kushindikana kuondolewa kwa kemikali ya potasiamu katika mirija ya damu husababisha mapigo ya moyo na kifo cha ghafla. Wakati mwingine dalili zinaweza zisijitokeze hata kama tatizo lipo. Dalili nyingine kwa wagonjwa ambao hawagunduliki mapema ni kuvimba macho wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye. Nyingine ni kuvimba miguu asubuhi na kupungukiwa damu mwilini ambazo huweza kujitokeza kama dalili za kwanza.

Post a Comment Blogger

 
Top