CHAMA  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani kimeanza kugawa  vifaa zikiwemo bendera kwa ajili maandalazi ya Umoja wa Kupinga Udikteta  ( Ukuta) ambayo yanatarajia kufanyika Septemba mosi mwaka huu.
Akizungumza  na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kanda ya  Pwani wa Chadema, Casimir Mabina, alisema kuwa bendera hizo zitaanza  kupeperushwa kuanzia kesho kutwa kwa ajili ya kuunga mkono azimio la  Kamati Kuu ya kufanyika oparesheni Ukuta.
Alisema  oparesheni Ukuta ni lazima ifanyike nchi nzima na kwamba hawako tayari  kuona ukandamizaji wa demokrasia unaoendelea kufanywa na serikali ya  awamu ya tano ambayo imeonyesha viashiria vya utawala wa kidikteta.
Alisema  Rais John Magufuli, anajaribu kuua demokrasia ya vyama vingi kwa  kukataza na kuzuia mikutano ya kisiasa ya vyama vya upinzani huku CCM  ikiendelea na mikutano yake kama kawaida.
“Tumeona  jinsi Rais alivyopiga marufuku wapinzani kukutana kwenye mikutano ya  hadhara huku akiwatishia kuwa wakikaidi atawashughulikia na kweli  amewaamuru polisi watekeleze amri hiyo ya kuwakamata viongozi wa Chadema  na kuwafungulia mashtaka,” alisema
Aliongezea  kuwa mbaya zaidi Jeshi la Polisi linazuia hata mikutano ya ndani ya  vyama vya upinzani na makongamano na hata mahafali ya wanafunzi wenye  itikadi za upinzani licha ya kutambua kuwa mikutano ya ndani haiwezi  kuleta uvunjifu wa amani kwa walio ndani ya ukumbi.
Alisema  licha ya kwamba Mwenyekiti wa CCM Rais Magufuli. amekataza mikutano  hiyo kufanyika chama tawala, kinafanya mikutano ya hadhara katika maeneo  mbalimbali kwa kisingizio cha shughuli za serikali.
Mabina  alisema juzi CCM ilisema itakuwa na maandamano kutoka uwanja wa ndege  wa Mwalimu Nyerere ya kumpokea Rais Magufuli hadi Makao Makuu ya CCM  yaliyopo Lumumba.
“Tunahoji  haki ya kufanya siasa ni kwa CCM tu na siyo kwa vyama vingine? Hili  jambo hatuwezi kukubali Jeshi la Polisi lituambie inakuwaje vibali  vinatolewa kwa CCM halafu upinzani tunyimwe tunasema lazima tufanye  oparesheni Ukuta ya kupinga ukandamizaji wa demokrasia,” alisema Mabina
Naye  Katibu wa Wabunge wa Upinzani Mkoa wa Dar es Salaam, Mbunge wa Viti  Maalum, Anatropia Theonest, alisema lengo la oparesheni ya Ukuta ni  kupinga ukandamizaji unaofanywa na serikali.

 
Post a Comment Blogger Facebook