WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani kwa watumishi wote wa sekta ya afya watakaobainika kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa ajili ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Pia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Stephen pamoja na Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. John Gurisha kusimamia na kulinda fedha za CHF zinazochangwa na wananchi na kuhakikisha zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye jimbo la Kwela, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga.
"Kitendo cha kula fedha zinazochangwa na wananchi kwa lengo la kupata huduma za afya kinawafanya wakatetamaa ya kuendelea kuchangia mfuko huo. Kama wako watumishi wenye tabia hizo waache mara moja," amesisitiza.
Mbali na kutoa agizo hilo kwa uongozi wa mkoa wa Rukwa, pia Waziri Mkuu amewataka wananchi kujiunga na CHF kwa sababu mfuko huo utawawezesha kupata huduma za matibabu bure wao na familia zao katika kipindi cha mwaka mzima.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze ye urefu wa kilometa 85 itajengwa kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika kwa urahisi na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati.
“Mimi nilidhani mlima wa Kitonga ndio mkali kuliko yote na eneo la Sekenke ndio linatisha zaidi!. Kumbe barabara ya kuja huku Mtowisa ndiyo inatisha zaidi kuliko zote. Lazima tuweke lami ili iendelee kupitika kwa urahisi zaidi,” amesema.
Akizungumzia ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Kwela, Ignas Malocha la kutaka tarafa hiyo ya Mtowisa kuwa wilaya au halmashauri, Waziri Mkuu amesema analichukua na kwenda kulifanyia tathmini na majibu atayapata kupitia uongozi wa mkoa.
Malocha alisema jimbo la Kwela linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara hali inayosababisha wananchi kushindwa kusafirisha mazao yao kwa urahisi.
Pia aliomba ukanda huo wa bonde la mto Rukwa upandishwe hadhi na kuwa wilaya au halmashauri ili kusogeza huduma za kijamii karibu na wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Rukwa, Mhandisi Masuka Mkina ameelezea mkakati wa kuboresha miundombinu ya barabara mkoani hapa ikiwemo ya kutoka Ntendo hadi Muze wilayani iliyopo wilayani Sumbawanga.
Mhandisi Mkina amesema Serikali imetenga jumla ya sh. milioni 170 kwa ajili ya kuweka zege kwa ajili ya kurahisisha upandaji wa mlima hasa kwenye eneo la Kizungu katika barabara ya kutoka Ntendo hadi Muze.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, AGOSTI 24, 2016.
Post a Comment Blogger Facebook