 WATU  watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wa kutumia silaha, ambao  wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu katika mkoa wa Dar es  Salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo la Vikindu wilaya ya  Mkuranga mkoani Pwani.
WATU  watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wa kutumia silaha, ambao  wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya kihalifu katika mkoa wa Dar es  Salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo la Vikindu wilaya ya  Mkuranga mkoani Pwani.Licha  ya kuuawa kwa majambazi hao, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es  Salaam, limefanikiwa kuwakamatwa watu zaidi ya saba, wanaosadikiwa  kuhusika na tukio la majibizano ya risasi na polisi, lililotokeo Vikindu  lililosababisha kifo cha askari mmoja.
Akizungumza  na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi  Kanda Maalumu, Simon Sirro alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao  walikamatwa katika maeneo tofauti ya Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.
Alisema  watu hao walikamatwa kufuatia tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29,  mwaka huu katika Jengo la Sophia House maeneo ya Veta Changombe, ambapo  majambazi hao walidaiwa kupora Sh milioni 35 na kutoweka kwa kutumia  gari aina ya Toyota Noah lenye namba bandia T 549 BPK.
Aliongeza  kuwa uchunguzi wa tukio hilo, uliendelea kufanyika na Septemba 3, timu  ya upelelezi kutoka Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, iliweka mtego na  kufanikiwa kuwakamata majambazi hao watatu na walipohojiwa walikiri  kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa kutumia silaha na kuweza  kutaja silaha mbalimbali walizonazo.
Kamanda  Sirro alisema majambazi hao, waliwapeleka askari eneo la Mbezi Chini  katika nyumba waliyokuwa wamekodi na askari walifanya upekuzi na  walifanikiwa kupata silaha mbalimbali, zikiwemo bunduki 23 na risasi  zaidi ya 800 na vitu vinginevyo.
Alitaja  silaha hizo kuwa ni bunduki za kijeshi tatu aina ya SMG zikiwa na  magazini nane na risasi 120, bastola 16, magazini tatu za bastola na  risasi moja, Shot gun pump action tatu na risasi 130, bastola 16  magazini na risasi 548 na bunduki tatu aina ya Shot gun na risasi zake  130.
Aidha  alisema walikuta redio za mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini  za kuonea mbali tatu, pingu za plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi  matatu, mkasi mmoja wa kukatia vyuma, mtarimbo mmoja, risasi baridi za  kutishia 37, boksi moja la kusafishia silaha, nyundo kubwa moja, pingu  za chuma tatu, mashine moja ya kuhifadhia kumbukumbu na magari mawili.
Alisema  uchunguzi wao ulibaini kuwa majambazi hao Septemba 6, mwaka huu  walipora bunduki aina ya Shot gun yenye namba 006091830, ikiwa na risasi  moja katika barabara ya Mbozi Chang’ombe.
Sambamaba  na hayo, majambazi hao walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha  katika Benki ya Habib African ya Kariakoo mwaka 2014 na Benki ya Stanbic  mwaka 2014, wakitumia gari aina ya Toyota Noah.
Kamanda  Sirro alisema baada ya mahojiano zaidi, majambazi hao walisema wanazo  silaha nyingine ambazo wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani  Pwani. Ndipo askari walifuatana na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa  Vikindu.
Alisema  askari walipofika eneo hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo,  walishuka kwenye gari na kuingia porini wakiwa wamewatanguliza  watuhumiwa mbele majira ya usiku.
Aliongeza  kuwa wakiwa msituni humo na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla  walisikia milio ya risasi ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini  na baadaye zikisikika sauti zikisema ‘mmetuua sisi’.
Alisema  baada ya risasi za mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao  ambao walichelewa kulala chini wakati risasi zikipigwa wakiwa  wamejeruhiwa sehemu za kifuani na tumboni huku wakivuja damu nyingi.
Alisema  askari walipiga risasi kuelekeza eneo zilikotokea risasi na  walipoendelea kusonga mbele, walikuta silaha aina ya SMG ikiwa  imetelekezwa na haikuwa na risasi ndani ya magazine, hivyo kufanya idadi  ya silaha za SMG kufikia nne.
Aidha  alisema askari waliwabeba majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari  kuelekea hospitalini, lakini wote walifariki dunia wakiwa njiani  kutokana na kutoka damu nyingi. 
Akizungumzia  tukio la Vikindu, Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao  wanaosadikiwa kuhusika na tukio ambalo lilisababisha kifo cha askari  mmoja.
“Majambazi  hao walikuwa ni kundi la kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya  saba ambao mpaka sasa tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha  upelelezi,” alisema Kamanda Sirro.
Pia  alisema kumekuwa na taarifa mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya  habari zikidai kuwa katika tukio la Vikindu, kuna askari anahusika na  tukio hilo na kudai taarifa hizo si za kweli na hakuna askari  aliyehusika katika tukio hilo.
Katika  tukio lingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa  makosa ya wizi wa magari manane, likiwemo gari moja la kibalozi. 
Kamanda  Sirro alisema magari hayo yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa  watu mbalimbali jijini hapo na mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea  kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu  tuhuma zinazowakabili.
Sirro  alisema katika tukio lingine jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata  watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na kuvunja nyumba usiku na kuiba. 



 
Post a Comment Blogger Facebook