Rais  wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit amemtumia ujumbe  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye  pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimuarifu kuwa hali ya  usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.
Rais  Salva Kiir Mayardit amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake  Maalum Mhe. Aggrey Tisa Sabuni ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo  amesema Sudani Kusini imekamilisha nyaraka za azimio la kuridia mkataba  wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umewasilishwa jana  tarehe 05 Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya Jijini Arusha.
Mhe.  Aggrey Tisa Sabuni amesema Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi  wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali  yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara na uwekezaji na kwamba ni  matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.
Kwa  upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za  kutengemaa kwa hali ya amani nchini humo na kwamba ni matarajio yake  kuwa Sudan Kusini itajikita katika maendeleo ya wananchi wananchi wake.
Katika  hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa  Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa  Rais huyo Mhe. Aime Laurentine Kanyana.
Katika  ujumbe huo Rais Nkurunziza amesema hali ya Burundi ni shwari na kwamba  wananchi wa Burundi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kwa  upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania yenye wakimbizi takribani  200,000 wa kutoka Burundi inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya  amani nchini humo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2016
Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea  ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Burudi uliowasilishwa kwake na Aime  Laurentine Kanyana Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Ikulu jijini Dar es  Salaam. Picha na IKULU 


 
Post a Comment Blogger Facebook