0
 
Dar es Salaam. Ni fainali leo pale vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapompitisha mgombea wake urais atakayepambanishwa na yule wa CCM, Dk John Magufuli aliyepitishwa Dodoma juzi.
Fainali hiyo ndani ya Ukawa inatarajiwa kuhitimisha mvutano uliokuwapo baina ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambaye tayari amechukua fomu kuwania urais ndani ya umoja huo na mgombea anayetajwa na Chadema, Dk Willibrod Slaa. Mwingine aliyechukua fomu katika umoja huo ni Dk Kahangwa wa NCCR-Mageuzi.
Yeyote atakayeibuka katika mpambano huo na kutangazwa rasmi leo, atakwenda kushindana katika fainali nyingine dhidi ya mgombea wa CCM katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
Wanaopewa nafasi ni Dk Slaa aliyegombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 2010 na kutoa upinzani mkali kwa Rais Jakaya Kikwete na Profesa Lipumba ambaye amejaribu bahati yake mara nne, 1995, 2000, 2005 na 2010 na sasa akitaka kujaribu kwa mara ya tano.
Wawili hao wameibua mvutano ndani ya vikao vya Ukawa na wajumbe wengi walikuwa wanaipa nafasi Chadema kusimamisha mgombea urais wa Muungano baada ya CUF kupewa nafasi ya kusimamisha mgombea urais Zanzibar.
Jumamosi iliyopita, kamati ya viongozi ya wakuu wa vyama vinavyounda umoja huo, NCCR-Mageuzi, Chadema, NLD na CUF ilikutana asubuhi na jioni kutoa tathmini ya walichokubaliana mbele ya wabunge wote na viongozi wa vyama hivyo kuwa mgombea wao atatangazwa leo.
Akitangaza uamuzi huo, Profesa Lipumba aliwaeleza waandishi wa habari kwamba kuna mambo ya kujadiliana baina ya vyama hivyo ila hayawezi kuleta matatizo, kwamba wapo pamoja na watatoa majibu ya pamoja.
Takriban wiki mbili sasa, viongozi wa Ukawa wamekuwa na mjadala mzito kuhusu kugawana majimbo ambayo mpaka sasa wamekubaliana kwa asilimia 97 na kushindwa kuafikiana kuhusu urais kutokana na mvutano kati ya Chadema na CUF.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliliambia gazeti hili jana kuwa kikao cha leo kipo palepale na kusisitiza kuwa bado wanaendelea na mazungumzo.
“Watanzania wasubiri kesho (leo) tutawaleleza kilichoafikiwa. Unajua kwenye siasa saa 24 zinaweza kuwa miezi 24. Siasa ni siasa na kila kitu kinawezekana katika siasa,” alisema.
“Kama tumeshawaambia watu kesho (leo) ndiyo tutazungumza, itabaki kuwa hivyo. Leo (jana) hatuwezi kusema chochote. Unajua tuna vitu vingi tunaendelea kuvikamilisha kwa sasa, tuvute subira na kila kitu tutakiweka wazi kesho,” alisema Mbowe.
Leo kabla ya kumtaja mgombea wa urais, viongozi wa Ukawa watakuwa na kikao cha majadiliano ambacho kitatoa mwelekeo wa umoja huo huku taarifa kutoka ndani ya vyama hivyo zikieleza kuwa mwafaka bado haujapatikana.

Post a Comment Blogger

 
Top