Dar es Salaam. Janeth Magufuli  bado anasubiri miezi mitatu ya kampeni nzito za kumuwezesha mumewe  kuingia kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, lakini walimu na wanafunzi wa  Shule ya Msingi Mbuyuni tayari wanasikitika kumpoteza mwalimu huyo wa  jiografia, historia na Tehama.
Mumewe, Dk John Pombe  Magufuli amepitishwa zaidi ya wiki moja iliyopita kuwa mgombea urais wa  Tanzania kwa tiketi ya CCM, na hivyo atalazimika kupambana vikali na  wagombea wa vyama vingine ili kujihakikishia anaingia Ikulu kuongoza  Serikali ya Awamu ya Tano.
Lakini walimu na wanafunzi  wa shule hiyo wanaona kuwa tayari Dk Magufuli ameshajihakikishia tiketi  ya kuingia Ikulu na walichonacho sasa ni kusononeka kwa kuwa wanampoteza  mmoja wa walimu bora shuleni hapo.
“Kama mumewe  akichaguliwa, nitakosa utu na busara zake. Na unajua? Ni mwalimu wa  mazingira na anajua majukumu yake. Darasa la tano watamkumbuka sana,”  anasema mwalimu mkuu wa shule hiyo, Dorothy Malecela.
“Ni  mwanamke mchapakazi sana na ni mwalimu mzuri, mtu mwenye upendo na  mnyenyekevu. mtu pia mwenye moyo mzuri. Wakati fulani alitoa msaada wa  baiskeli kwa mwanafunzi mlemavu shuleni hapa.”
Alikuwa  akimzungumzia mwanafunzi mlemavu Elisha Lameck, ambaye alikuwa akipata  shida kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakati akiwa shuleni hapo.
Mwalimu Malecela anasema licha ya kuwa ni mke wa Waziri Magufuli, ilikuwa kazi kufahamu kama ni mke wa kigogo.
“Hakuwa  na makuu hata kidogo, hata watoto wake walikuwa wakisoma hapa, na  mwingine anasoma shule ya Kata ya Oysterbay,” anaeleza.
“Watoto wao wanasoma shule za kawaida sana. Shule ya kata tofauti na wengine ambao huwapeleka nje ya nchi.”
Malecela alieleza kuwa Mwalimu Magufuli hakuwa mtegeaji kazini.
“Hakuwahi kukosa kipindi na kama akiwa na dharura huwa anamwomba mwalimu mwingine amsaidie kipindi chake,” alisema.
Si mwalimu mkuu pekee ambaye alimmwagia sifa Mama Magufuli.
Ally  Rajab na John Manda, ambao wako naye ofisi moja wanamuelezea Mwalimu  Magufuli kuwa mtu ambaye ilikuwa vigumu kumtambua kuwa ni mke wa waziri,  lakini pia mpole na anayeipenda kazi yake.
Mwalimu  Rajab alisema kuwa wakati mwingine walikuwa wakinunua mihogo na kachori  kwa ajili ya chai asubuhi, na Mwalimu Janeth alikuwa akijumuika kula  pamoja nao.
“Hata wakati mwingine wa safari za mafunzo, huwa anatoa fedha kwa watoto ambao wazazi wao wameshindwa kuwalipia,” alisema.
“Hata wakati mwingine inapotokea walimu kukwaruzana ofisini, amekuwa msuluhishi.”
Baadhi  ya wanafunzi wa shule hiyo, Mabano Mzee, Mariam Mwalami wanafunzi wa  darasa la sita, wanasema kuwa Mwalimu Magufuli alikuwa wa aina yake.
Mzee anasema mke huyo wa Dk Magufuli si mtu wa kuchapa viboko wanafunzi.
“Kama kuna tatizo, anakuelekeza, kama una shida anakusikiliza,” alisema Mzee.
Naye  Mariam anasema kuwa anampenda Mwalimu Magufuli kwa kuwa anajua jinsi ya  kumfundisha mtu na anaelewa, na huwa anajua kama watu wameelewa ama la.
“Baada  ya kufundisha huwa anamwita mwanafunzi na kumuuliza kama ameelewa na  kinachonifurahisha, hata tunapokula makande naye hula,” alisema Mariam.
Stella  Ijumba, mwalimu na rafiki mkubwa wa Janeth Magufuli, anasema aliposikia  Dk Magufuli amepita, alijua hatakuwa tena na mwalimu huyo.
“Niliposikia  mzee kapita, nikamtumia meseji, ‘Hongera rafiki yangu, hayo yote  yamepangwa na Mungu’, japokuwa hakujibu, lakini nilijua tu wengi  watakuwa wamemtumia sasa anashindwa kujibu, alisema mwalimu huyo wa  darasa la nne.
“Nitamkumbuka sana rafiki yangu, alikuwa mpole sana... ninawatakia kila la kheri yeye na mumewe.”
Mwingine  aliyemzungumzia Mwalimu Magufuli ni muuza matunda shuleni hapo, alisema  kuwa atamkosa mteja wake ambaye mara kwa mara hununua matunda kwa ajili  ya kula ama kupeleka nyumbani.
“Huwa napeleka matunda  hata nyumbani kwake huwa ananiagiza, lakini juzi juzi hapa nilipokwenda  nikakuta hali tofauti, kulikuwa na ulinzi mkali, nikashindwa kumuuzia,  nikaondoka,” alisema muuza matunda huyo.
“Baadaye  nikasikia habari za mumewe kuwa ameteuliwa kuwania urais, nikaona sasa  ni ngumu tena kumuona na itakuwa tunamuona kwenye Tv tu.”
Lameck,  ambaye alinunuliwa baiskeli na Janeth alisema: “Ninampenda sana Mwalimu  Magufuli kwani kanisaidia baiskeli hii...mama huwa ananichukua kunileta  shule, lakini hii imenisaidia na itampunguzia mama kazi,” anasema.
Anasema  kuwa kaka yake, Eliya sasa ndiye anayemsindikiza kutoka na kwenda shule  na mama yao amebaki nyumbani akiendelea na shughuli nyingine.
Iwapo  Dk Magufuli atachaguliwa kuliongoza Taifa Oktoba 25, Shule ya Mbuyuni  itakuwa imeweka historia ya aina yake kwa kutoa wake wawili wa marais.
Salma  Kikwete, mke wa Rais anayemaliza muda wake, pia alifundisha shule hiyo  katika kipindi chake cha miaka 20 ya utumishi serikalini.
Lakini  kingine kitu kingine cha aina yake ni kwamba iwapo Dk Magufuli atakuwa  Rais, maana yake mkewe ataingia kwenye kundi la wake za marais wawili wa  nchi zilizo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao majina yao ni  Janeth.
Mke wa Rais wa Uganda ni Janet Kataaha Museveni wakati mke wa Rais Paul Kagame wa Rwanda anaitwa Jeannette Kagame.
Post a Comment Blogger Facebook