Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Awamu ya Pili,  Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa shughuli ya kupata mgombea urais  kwa tiketi ya CCM haikuwa rahisi na akashukuru kwamba imemalizika kwa  amani.
Mchakato huo ulihitimishwa Julai 12 mjini Dodoma  wakati Mkutano Mkuu wa CCM ulipopitisha jina la Dk John Magufuli  kugombea nafasi ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais  Jakaya Kikwete kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka.
Jumla  ya makada 38 walijitokeza kuwania nafasi hiyo, na majina matano ndiyo  yaliyopitishwa kwenda Halmashauri Kuu na baadaye matatu kwenda Mkutano  Mkuu.
Mchakato wa urais ndani ya CCM ambao kwa kawaida  hutawaliwa na msuguano kabla ya kumalizika kwa maridhiano, safari hii  ulienda mbali zaidi baada ya wajumbe watatu wa Kamati Kuu kupinga nje ya  kikao uamuzi wa chombo hicho na baadaye wajumbe wa Halmashauri Kuu  kumwimbia mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete wimbo wa kuonyesha wana imani  na Edward Lowassa baada ya jina la mbunge huyo wa Monduli kuenguliwa na  Kamati Kuu.
Jana, akitoa hotuba fupi baada ya  kumalizika kwa sala ya Eid el Fitr kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini  Dar es Salaam, Mwinyi alizungumza kwa mara ya kwanza hadharani kuhusu  mchakato huo, akidokeza hali ilivyokuwa.
“Haikuwa kazi  rahisi kwenye mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha  bendera ya CCM,” alisema Mwinyi lakini akawahi kuipoza kauli hiyo kwa  kuelezea amani ilivyotawala mwishoni.
“Kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.”
“Uchaguzi  huu ni kwa ajili ya kuwapata viongozi wetu, tunataka viongozi bora wa  kutuletea maendeleo, mapatano na wenye mahaba na wananchi.”
Akizungumza  hadharani kwa mara ya kwanza baada ya mchakato huo wa kumtafuta mgombea  wa urais kukamilika mjini Dodoma, Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu kwa  mchakato huo kuisha salama.
“Haikuwa kazi rahisi kwenye  mchakato huu wa kumtafuta mgombea mmoja atakaye peperusha bendera ya  CCM, kama ni jahazi basi sasa tunashukuru limefika pwani salama.
“Sasa,  ninawaomba Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi wa  nchi tunaoufanyika kila baada ya miaka mitano,“ alisema Rais Mwinyi  ambaye alikuwa mmoja ya wajumbe wa Baraza la Ushauri waliofanya kazi ya  kutuliza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM hadi kuafikiana kuendelea na  mchakato wa kumpata mgombea urais.
Aliwasisitizia  Watanzania kuacha tabia ya kupenda mno na kuacha kubaguana, akisema  hakuna aliye bora na kuwataka kuzidisha mapenzi miongoni mwao na  kusherehekea vyema Sikukuu ya Eid el Fitr. “Hakuna jambo lenye maana  kama hili la kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kutufikisha salama siku  kama hii ya leo (jana) ambayo tunasherekea Sikukuu ya Eid,” alisema  Mwinyi.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad  Mussa Salum aliwasisitizia wananchi umuhimu wa kusherekea sikukuu hiyo  katika hali ya amani na utulivu.
Pia, aliwashauri  wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao sehemu zenye maadili ili  washerehekee kama ambavyo Mwenyezi Mungu anapenda.
“Leo  (jana) ni siku ya furaha, naomba tusherekee maeneo salama pia Waislamu  msisahau kufunga sita kwani ina malipo makubwa,” alisema Alhad Salum.
Mkoani  Geita ambako ilifanyika sala ya kitaifa ya Eid, Makamu wa Rais, Dk  Mohamed Gharib Bilal alihutubia Baraza la Eid na kusema kipindi hiki  kinahitaji utulivu, kuelewa na kuheshimiana pamoja na kudumisha uhusiano  ili Taifa lipate viongozi bora.
“Tuwe watulivu ili  Tanzania ibaki kuwa nchi ya kukimbiliwa na isiwe nchi ya kukimbiwa...  sisi tusiwe wakimbizi, tuwe watu wa kupendana, kuvumiliana na  kuthaminiana. Tusifikie hatua ya kuchukiana, kuuana na kufanyiana  ukatili,” alisema Dk Bilal.
Alisema amani inaweza  kuvunjwa na mtu yoyote kwa namna yoyote ile, akaharibu mazuri na heshima  ya Taifa na akawaomba wananchi na waumini wote wasifikie hatua hiyo  akisema ndiyo wenye uwezo wa kuifanya nchi yao kuwa ya amani.
“Tuishi  kwa kuheshimiana, kupendana na kuvumiliana tushikamane katika, hali  iliyopo sasa kwa nchi yetu siyo nzuri. Si ajabu hivi sasa tunavyoongea  kuna sehemu mabomu yametokea, si ajabu kuna watu wameuawa kikatili. Hii  yote ni sababu watu sasa wanapoteza misingi ya kuheshimiana, upendo na  kuvumiliana,” alisema Bilal kwenye Viwanja vya Karangara.
Awali  Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania, Bakwata, Sheikh Suleiman  Lolela alisema waumini na wananchi wote waitumie vyema nafasi ya  Uchaguzi Mkuu kuhakikisha wanachagua viongozi bora watakaoendeleza  amani.
Kisiwani Unguja, Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed  Shein amewataka viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za kijamii na  madhehebu ya dini kulinda na kuheshimu msingi na malengo ya kuanzishwa  Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) wakati huu wa kuelekea Uchaguzi Mkuu  unaotarajiwa kufanyika Oktoba.
Akiuhutubia kwenye  Baraza la Eid el Fitr lililofanyika Ukumbi wa Bwawani na kuhudhuriwa pia  na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad jana, Dk Shein  alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kufanya siasa kwa kuzingatia  misingi ya Katiba na sheria kwa madhumuni ya kuendeleza na kulinda amani  na umoja wa kitaifa kwa manufaa ya Zanzibar na wananchi wake.
“Tunaweza  kushindana bila ya kulaumiana, kukejeliana na tunaweza kushindana bila  ya kudharauliana au kuhasimiana,” alisema Dk Shein kwenye shughuli hiyo  iliyotaliwa na hali ya utulivu.
Alieleza kuwa vyama vya  siasa vimeanzishwa na vipo kwa ajili ya kushindana kwa sera kwa  madhumuni ya kuchochea maendeleo ya Zanzibar na siyo kugombanisha watu  na kuvuruga misingi ya amani na umoja wa kitaifa.
Kwenye Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, sheikh wa mkoa, Ahmed Zuber aliwataka Watanzania kudumisha amani na umoja.
Zuber  alisema dunia sasa imechafuka kutokana na uvunjifu wa amani  unaochochewa na siasa chafu hivyo Watanzania bila kujali dini wala  itikadi zao wanapaswa kuilinda amani iliyopo sasa.
“Tunahitaji  utulivu. Nchi nyingi huharibikiwa kipindi kama hiki cha uchaguzi, amani  hupotea kipindi hiki cha uchaguzi. Ndugu zangu Waislamu na msio  Waislamu tukiichezea amani hii iliyopo sasa, tujue hakika hatuna kwa  kukimbilia,” alisema.Mkoani Tanga, imamu wa Msikiti wa Ibadhi, Sheikh  Mohammed Said aliitaka jamii kudumisha amani na utulivu uliopo na kuacha  kushabikia vyama vya siasa.
Sheikh huyo alisema ni  wajibu wa kila mtu kutambua kuwa amani iliyopo ikitoweka ni vigumu  kuirejesha na hivyo kila mmoja ahakikishe anatambua wajibu wake.
Alisema  wakati wa uchaguzi, hutokea jamii kuhamasishana kwa mambo ya kisiasa,  jambo ambalo alisema ni baya na halifai kutokea na hivyo kutaka kila  mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake.Mkoani Lindi, Sheikh Salimu Nalinga akitoa  salamu za Eid el Fitr aliwataka Waislamu kuchagua viongozi waadilifu  ili kuifanya nchi kuendelea kuwa ya amani na utulivu.
Post a Comment Blogger Facebook