0
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, (NEC) Jaji Damian Lubuva amesema mgombea urais mteule wa CCM, Dk John Magufuli hapigi kampeni bali kinachofanyika ni utambulisho wa mgombea wao kwa wananchi.
Kauli ya Lubuva imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Chama cha ACT-Wazalendo kuandikia barua NEC, ikilalamika kuwa Dk Magufuli ameanza kampeni kabla ya wakati.
Alisema NEC imepokea barua ya malalamiko ya ACT-Wazalendo inayolalamika kuwa Magufuli ameanza kampeni kabla ya muda na pia kulalamika kualikwa kwa mteule huyo wa CCM kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Michuano ya Kombe la Kagame, inayoanza leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
“Tume ina maadili yake, kwa mfano eti tumzuie asiende kwenye mechi , sisi tumzuie kama nani, huu si wakati wetu, wakati wetu ukifika tutakunjua makucha yetu” alisema.
 Alisema NEC haihusiki hata  na yale yanayotokea Dodoma,  bali itaanza kazi yake ifikapo Agosti 21 mara baada ya uteuzi rasmi wa wagombea.
Akizungumzia zaidi ziara hizo, Jaji Lubuva alisema tume hiyo haina kauli juu ya ziara ya Magufuli, bali akifanyacho ni mchakato tu wa ratiba ya chama chake.
 Jaji Lubuva alisema  kwa upande wa Sheria na Katiba, Nec itaanza kuchukua hatua kwa wale watakaokiuka kanuni kuanzia Agosti 22, pindi kipyenga cha kampeni kitakapoanza hadi Oktoba 24 kitakapomalizika.
“Katika kipindi hicho, tume inakuwa na nguvu ya kuwashughulikia wagombea, kwa sasa kinachotokea ni mambo ya vyama, sisi kwenye tume hatuna msingi wa kushughulikia hayo,” alisema.
Wakati Jaji Lubuva akisema hayo, Chama Cha Kijamii (CCK) wameamua kutumia wanasheria ili kuandaa mipango ya kumwekea pingamizi Dk Magufuli, kuwa anakiuka Sheria ya Uchaguzi kwa kufanya kampeni kabla ya wakati.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa CCK Renatus Muhabi, alisema Tume ya Uchaguzi (NEC) huenda nayo ikashtakiwa kwa kushindwa kuwajibika licha ya kuwa ndiyo msimamizi wa Sheria ya Uchaguzi.
“Tumeshampa kazi mwanasheria, Aloys Rugazia kuandaa pingamizi baada ya kutoridhishwa na majibu ya Jaji Lubuva.
“ Majibu yake Jaji Lubuva ni wazi yanaonyesha kuwa anaiogopa CCM, maana ndiyo iliyompa hiyo nafasi, hapo unaweza kuona kwa nini tumekuwa tunalilia tume huru, yeye anapodai hahusiki na kufuatilia mambo anayofanya mgombea huyo, eti hadi pale atakapochukua fomu ya NEC, huu siyo utawala bora ni ukiukwaji mkubwa,” alisema.

Post a Comment Blogger

 
Top