0
ZITTO Kabwe, kiongozi mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, amepata mapigo mawili kwa mpigo ndani ya kipindi cha wiki moja.

Kwanza, chama chake kimezuiwa kujiunga na Jumuiko la vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na pili; kimeachwa njiani na waliowaita, “wabunge 50 watakaojiunga na ACT mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge.”

Taarifa kutoka ndani ya UKAWA zinasema, Zitto na chama chake wamezuiwa kujiunga na umoja huo kwa hofu ya kutoa siri za viongozi wakuu wa vyama hivyo na kisha kuzikabidhi kwa Rais Jakaya Kikwete na chama chake cha CCM, MAWIO limeelezwa.

Zitto amekuwa akitajwa kuwa swahiba mkubwa wa Rais Kikwete na baadhi ya maofisa wa usalama wa taifa wanaomtumia kupata taarifa za upinzani, kuvuruga vyama na kuchonganisha viongozi wakuu wa chama na wanachama.

Kupatikana kwa taarifa kuwa viongozi wa UKAWA wamegoma kumruhusu Zitto kujiunga na umoja huo, zimekuja wiki mbili baada ya gazeti hili kuripoti kuwa mwanasiasa huyo amekuwa akitumia kampeni chafu za kidini, kunadi chama chake.

Akiwa katika ziara ya kutambulisha anachoita chama chake, Zitto alisikika akitamba majukwaani mkoani Kigoma, kuwa “ACT ni chama cha Waislamu.”

ACT- Wazalendo kiliwasilisha barua kwa makatibu wakuu wa vyama vinne vinavyounda UKAWA, kikiomba kujiunga navyo kwa kile kilichoita, “kuongeza nguvu ya kuiondoa CCM madarakani.”

Hata hivyo, Ofisa Habari wa ACT, Abdallah Hamisi amekana chama chake kuwasilisha maombi ya kujiunga na umoja huo.

“Kwanza ieleweka, kwamba ACT haijawahi kuandika barua kuomba kujiunga na UKAWA. Sisi tuliandika barua kuomba kujua sifa ya vyama vinavyotaka kujiunga na umoja huo,” anaeleza.

Anasema, “ACT iliandika barua kutaka kujua utaratibu wa kujiunga na umoja huo. Tulifanya hivyo kwa kuwa hatukujua nani hasa anapaswa kuandikiwa barua kama kiongozi mkuu wa UKAWA.”

Abdallah anakiri kuwa mpaka juzi Jumanne, barua aliyodai ililenga kutaka kufahamu taratibu za kujiunga na umoja huo; ilikuwa haijajibiwa na chama chochote kilichomo katika muungano huo.

Muungano wa UKAWA unaundwa na vyama vya NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na National Democrat Party (NLD).

Hofu ya UKAWA inatokana na safari ya miaka 10 ya kisiasa ya Zitto ndani ya Chadema; ambayo iliishia kwa tuhuma za usaliti; kushirikiana na baadhi ya wanachama waliokuwa mstari wa mbele kuvuruga chama hicho na kusababisha migogoro isiyoisha ndani ya chama.

Zitto alituhumiwa kushirikiana na wanaotaka kuangamiza maisha ya viongozi wakuu wa chama hicho na maadui wa chama.

Ndani ya Chadema, Zitto alituhumiwa kuzunguka nchi mzima kuunda mtandao wa kusaka uenyekiti wa chama hicho; na kuhujumu baadhi ya wenzake ndani ya chama ili kujinufaisha binafsi.

Barua ya ACT -Wazalendo, kwenda kwa makatibu wakuu wa Chadema, NLD, CUF na NCCR- Mageuzi, kuomba kujiunga na UKAWA, iliandikwa 25 Aprili mwaka huu. Ilisainiwa na Samson Mwigamba, katibu mkuu wa chama hicho.

Mwigamba alithibitisha kuandikwa kwa barua kwenda kwa vyama vinne vinavyounda UKAWA.

Alisema, malengo ya barua yao yalikuwa mawili; “moja ni kueleza nia ya kutaka kujiunga na umoja huo; na pili, kuuliza ni taratibu zipi zinatakiwa kufuatwa kabla ya chama kuruhusiwa kujiunga na umoja huo…”

Kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya UKAWA ameliambia MAWIO kuwa kinachozuia Zitto kuingizwa ndani ya umoja huo, ni hofu ya viongozi wakuu kuwa aweza kusababisha mgogoro, ambao umoja unaweza kuvunja umoja huo.

Vyanzo vya taarifa kutoka ndani ya ACT vinasema, matumaini ya wanachama na wapenzi wa Zitto kuvuna wabunge wa CCM, yamezimika mwishoni mwa wiki iliyopita, baada ya baadhi ya wabunge waliotarajiwa kujiunga na chama hicho, kuendelea kubaki CCM na wengine kutimkia Chadema.

Wabunge ambao walitatarajiwa kujiunga na ACT, lakini wakaamua kukitosa chama hicho dakika za mwisho, ni pamoja na Deo Filikunjombe, James Lembeli na Kangi Lugola, wote kutoka CCM.  Wengine, ni Said Alfi na John Shibuda (Chadema).

Lembeli tayari ametangaza kujiunga na Chadema. Naye Lugola anatarajiwa kujiunga na chama hicho leo mjini Mwanza.

Kwa upande wa Filikunjombe ambaye ni swahiba mkubwa wa Zitto, tayari amerejesha fomu yake ya ubunge kupitia chama chake – CCM.

Aidha, Zitto “aliwekeza” kwa John Shibuda akiahidi kuwa angejiunga na chama chake.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, jijini Dar es Salaam, Aprili mwaka huu, kiongozi huyo mkuu wa ACT , alijitapa kuwa zaidi ya wabunge 50 wa vyama mbalimbali vya siasa nchini watajiunga na chama hicho kipya ili kugombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.

Zitto ambaye alifukuzwa uanachama wa Chadema, alidai kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana.

Alisema, “…tuna wagombea ubunge wengi wakiwamo wabunge wa sasa ambao katika uchaguzi mkuu wa Oktoba hawatagombea kupitia vyama vyao vya sasa.

“Wapo ambao hawatakwenda hata katika kura za maoni za vyama vyao na wameshafanya uamuzi. Wote hawa watajiunga na ACT,” alisema.

Ni Moses Machari, aliyekuwa mbunge wa Muhambwe (NCCR- Mageuzi), ndiye pekee aliyejiunga na Zitto.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, pigo kubwa ambalo Zitto amelipata ni hatua ya Alfi kukimbilia CCM.

Alfi na Zitto wote walikuwa viongozi waandamizi ndani ya Chadema. Wakati Zitto akiwa naibu katibu mkuu, Alfi alikuwa makamu mwenyekiti. Alijiuzulu siku moja baada ya Zitto kuvuliwa nyazifa zake zote ndani ya Chadema

Post a Comment Blogger

 
Top