0
 Ni kichekesho na Serikali kuahidi kwa wazanzibari kuwa mafuta na gesi sio suala la Muungano halafu inatunga sheria za mafuta na gesi za kutumika Zanzibar. Miswada hii haikufikiriwa vizuri na hivyo iondolewe.

Muswada wa mafuta na gesi Asilia hauzingatii haki za wananchi. Imerundika mamlaka kwa Waziri wa Nishati na Madini na haki ya wananchi kushiriki na kutoa ruhusa utafutaji na uchimbaji haikuainishwa kwenye sheria. Chama cha ACT Wazalendo kinataka haki hii iwepo kwenye sheria.

Haki ya ' free prior informed consent ' ni suluhisho la migogoro kati ya wananchi na wawekezaji.

Muswada wa mapato ya mafuta na gesi imeandikwa haraka haraka na umeacha kabisa kushughulikia suala la mgawo wa mapato ya mrahaba kwa maeneo yenye utajiri huo.

Kwa miaka mingi tumekuwa tukipendekeza kuwa sehemu ya mapato, hasa mapato kutoka kwenye mirahaba ibaki kwenye wilaya zenye rasilimali.

Muswada huu umekwepa eneo hilo na litaleta mgogoro mkubwa kwenye nchi yetu. Hivi sasa wananchi wanaotoka kwenye maeneo yenye Dhahabu wanapata mgawo kutoka tozo za halmashauri.

Muswada huu upo kimya eneo hilo na hivyo kukosesha mikoa kama Mtwara chanzo muhimu cha mapato.

Muswada huu ukienda bungeni bila kupata maoni ya watu wa Kusini itakuwa sio haki. Ni vema kuondoa muswada huu bungeni ili kupata muda wa kutosha wa kupata maoni ya wananchi.

Wananchi wa Mtwara, chama cha ACT Wazalendo ndio chama pekee cha siasa hapa nchini ambacho kimeweka wazi sera zake kuhusu utajiri wa Maliasili ya nchi.

Sera hizo zimetamkwa ndani ya Azimio la Tabora lililozinduliwa tarehe 13 Juni 2015 mjini Tabora.

Azimio lina lengo la kuhuisha Azimio la Arusha ili kujenga Tanzania ya watu walio sawa na wananchi kumiliki uchumi wao wenyewe.

Tumewaletea chama chenu, mkipokee na kukilea. Chama cha Wanyonge chenye misingi imara na shabaha ya kuwakomboa watanzania kiuchumi.

Asante sana
Zitto Kabwe
Kiongozi wa ACT Wazalendo

Post a Comment Blogger

 
Top