0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Agosti 4, 2015, ametia saini Miswada ya Sheria mitano hadharani ikiwa ni hatua yake ya mwisho kabisa kuridhia Miswada ya Sheria akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika sherehe iliyofanyika katika Ukumbi mpya wa Ikulu, Dar Es Salaam,Rais Kikwete ameridhia Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesiasilia, Muswada wa Uwazi na Uwajibikaji, Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesiasilia, Muswada wa Masoko ya Bidhaa na Muswada wa Tume ya Walimu.

Katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na mamia ya wageni waalikwa, mawaziri wanaohusika na sekta hizo, Mheshimiwa George Simbachawene ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Saada Mkuya ambaye ni Waziri wa Fedha na Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa ambaye ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wametoa maelezo ya miswada hiyo mitano kabla haijaridhiwa na Rais Kikwete.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue pia wamehudhuria sherehe hizo ambazo vile vile zimehudhuriwa na mawaziri wa Serikali, mabalozi, wawakilishi wa taasisi zisizokuwa za Kiserikali (NGO’s) na wadau wengine wa sekta ambazo Miswada yake imeridhiwa.

Hiyo ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuridhia Miswada ya Sheria hadharani. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 wakati Rais Kikwete aliporidhia hadharani Muswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha katika Uchaguzi.

Aidha, hiio ni mara ya mwisho kwa Rais Kikwete kuridhia Miswada ya Sheria nchini kabla ya kuondoka madarakani mwanzoni mwa Novemba, 2015. Rais tayari amelivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini hati ya Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesiasilia Jumanne, Agosti 4, 2015 katika Ukumbi mpya wa Ikulu, Dar Es Salaam akishuhudiwa na Waziri wa Nishati na Madini Mhe George Simbachawene na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Ngosi Mwihava

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini hati ya Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesiasilia Jumanne, Agosti 4, 2015 katika Ukumbi mpya wa Ikulu, Dar Es Salaam akishuhudiwa na Waziri wa Nishati na Madini Mhe George Simbachawene na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Ngosi Mwihava.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini kuridhia Muswada wa Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesiasilia Jumanne, Agosti 4, 2015 katika Ukumbi mpya wa Ikulu, Dar Es Salaam akishuhudiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya na Katibu Mkuu wizara hiyo Dkt. Servacius Likwelile.

Post a Comment Blogger

 
Top