Walipoombwa kutaja moja kwa moja jina la mgombea Urais ambaye wangemchagua, asilimia 65 ya wananchi walimtaja mgombea wa CCM, John Magufuli. Asilimia 25 walimtaja mgombea wa Chadema (na Ukawa), Edward Lowassa. Asilimia 10 iliyosalia iligawanyika kati ya wale waliomtaja mmoja miongoni mwa wagombea urais wengine, waliokataa kujibu na waliokuwa bado hawana mgombea waliyempendelea. Hata hivyo, takwimu zilikusanywa kabla vyama vingine, kikiwemo ACT-Wazalendo, kuteua wagombea wao wa Urais. Takwimu hizi (zilizokusanywa kati ya Agosti na Septemba) sio utabiri wa matokeo ya uchaguzi. Zinaonyesha tu kwamba mwanzoni mwa kipindi cha kampeni, mgombea Urais wa CCM, John Magufuli, alikuwa anaongoza katika kura za maoni.
Aidha, vigezo muhimu vinavyohusu makundi mbalimbali ya watu (demografia) vilitumika kuchambua ni nani au makundi gani yanayowaunga mkono John Magufuli na Edward Lowassa. Wahojiwa ambao walikuwa vijana zaidi, wasomi zaidi, wanaume na wakazi wa mijini, walimuunga mkono Edward Lowassa. Makundi ya wahojiwa wazee zaidi, waliokuwa na elimu ya msingi tu, wanawake na wakazi wa vijijini walielekea kumuunga mkono zaidi John Magufuli kuliko vijana zaidi, wasomi zaidi, wanaume au wanaoishi mijini.
Hata hivyo, katika makundi yote haya, John Magufuli wa CCM anaonekana kuongoza. Kwa mfano, asilimia 33 ya wananchi wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 30 ya wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Lowassa, tofauti na asilimia 15 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 50. Pamoja na hayo, asilimia 57 ya watu wenye umri wa 18 – 29 na asilimia 76 ya watu wenye umri wa 30 – 39 wanamuunga mkono Magufuli. Upande wa makazi, asilimia 28 ya wakazi wa mijini walimuunga mkono Edward Lowassa tofauti na asilimia 24 ya wakazi wa vijijini. Asilimia 66 ya wakazi wa vijijini na asilimia 61 ya wakazi wa mijini wanamuunga mkono John Magufuli.
Asilimia 26 ya wanaomuunga mkono John Magufuli walidai kwamba ni kwasababu yeye ni mchapakazi, na asilimia 12 ya wanaomuunga mkono Edward Lowassa walisisitiza kwamba anaweza kuleta mabadiliko yanayohitajika nchini. Izingatiwe kwamba kauli hizi zinafanana karibu neno kwa neno na kauli mbiu za kampeni za wagombea hawa wawili.
Hata hivyo, wananchi hawana taarifa sahihi juu ya nafasi rasmi ya Ukawa kama mseto. Asilimia 49 ya wananchi wanafikiri kwamba Ukawa ni chama cha siasa kilichosajiliwa, kinyume na hali halisi. Asilimia 57 wanafikiri kwamba neno ‘Ukawa’ litakuwepo kwenye karatasi zao za kupigia kura. Hii pia, sio kweli. Bila kampeni na juhudi za kuwaelimisha wapiga kura ili wawe na taarifa sahihi kuhusu jambo hili, hali hii inaweza kuleta wasiwasi siku ya uchaguzi.
Matokeo haya yalitolewa na Twaweza katika muhutasari wa utafiti mwenye jina la Sema mwananchi, sema | Maoni ya wananchi kuhusu uongozi wa kisiasa. Muhtasari huu umetumia takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika unaotumia simu za mkononi na wenye uwakilishi wa taifa zima. Matokeo yanatokana na Awamu ya 1 ya kuwapigia simu wahojiwa wapya 1,848 iliyoendeshwa kati ya Agosti na Septemba 2015. Wahojiwa waliteuliwa kwa kutumia njia kama zinavyotumika na asasi za utafiti duniani kote. Unasibu (sampling) huu ulifanyika katika mikoa yote ya Tanzania Bara. Takwimu hizi zimelinganishwa na zile za awamu za utafiti katika miaka ya nyuma, zikiwemo:
- Utafiti wa awali wa kwanza wa Sauti za Wananchi 2012
- Sauti za Wananchi Awamu ya 10 ya Octoba 2013
- Sauti za Wananchi Awamu ya 24 ya Septemba 2014
- Awamu za utafiti za Sauti za Wananchi Aprili-Julai 2015
- Utafiti mpya wa awali ulioendeshwa kati ya Julai na Agosti 2015
Asilimia 64 ya wananchi walisema kwamba wanakumbuka vyema ahadi zilizotolewa na Wabunge wao katika uchaguzi uliopita, na asilimia 86 kati ya hao walisema kwamba mbunge wao hakutekeleza ahadi hizo au alizitekeleza chache.
Aidha, wananchi waliorodhesha changamoto kuu walizoona hapa nchini. Kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, huduma za afya ni changamoto kwa asilimia 59 ya Wananchi, ukosefu wa maji ikitajwa na asilimia 46, elimu duni na asilimia 44, na umaskini, asilimia 39. Hata hivyo, kumekuwa na mabadiliko kadhaa. Watu wachache zaidi walitaja umaskini (wamepungua kutoka asilimia 63 mwaka 2014) na watu wengi zaidi walitaja maji (wameongezeka kutoka asilimia 27 mwaka 2014).
“Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia hapa,” alisema Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza. “Wananchi wanabadilisha mawazo kuhusu vipaumbele vyao. Waliweka kipaumbele kwa afya badala ya umasikini katika kipindi kifupi cha miezi 12.”
“Watu wana hamu kubwa sana ya kupiga kura” aliongeza, “lakini hali hii si kigezo cha kuaminika katika kutabiri wangapi kweli watapiga kura siku ya uchaguzi. Wakijitokeza kwa wingi, itaipa uhalali mkubwa serikali ya awamu ijayo. Wakijitokeza wachache, inaweza kuashiria ama hali ya wananchi kukata tamaa, au hali ya kujiamini kwamba tayari wameshinda, au hali zote mbili kwa pamoja.”
“Kwa pamoja, mambo haya mawili yanatoa picha kwamba huenda wapiga kura wakawa hawana uhakika wamchague nani. Yanaimarisha ujumbe kwamba mashindano haya ndio kwanza yameanza kupamba moto. Wagombea hawana budi kuimarisha mahusiano yao na wapiga kura wakiwa na malengo mawili makuu; Lengo la kwanza ni kunadi ubora wa ilani na sera zao. Lengo la pili ni kuhakikisha kwamba watajitokeza kwa wingi kuwapigia kura siku ya uchaguzi, Oktoba 25.”
Post a Comment Blogger Facebook
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.