0
Baadhi ya wanachama wa Chadema wilayani Ludewa wakiwa na mabango wakati wa maanadamano leo.

WANACHAMA zaidi ya 500 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilayani Ludewa Mkoani Njombe wamekihama chama hicho na kujiunga na chama cha ACT Wazalendo wakipinga hatua ya uongozi wa juu wa chama hicho kukata jina la mshindi wa kwanza wa kura za maoni Bw. Ocol Haule na kumteua aliyekuwa mshindi wa pili katika mchakato huo Bw Bartholomeo Mkinga .
Wanachama hao ambao kutoka kata mbalimbali za wilaya ya Ludewa wamefanya maandamano hayo ya amani leo kuelekea ofisi ya Chadema wilaya huku wakitishia kuichoma moto ofisi hiyo baada ya viongozi wake kuifunga, kuitelekeza na kukimbia kunusuru maisha yao.
Wakizungumzia hatua hiyo ya kupinga maamuzi ya chama ngazi ya taifa wanachama hao Bi Hongera Gama, Taukile Mapunda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (BAWACHA) wilaya ya Ludewa Bi. Sophia Mtega walisema kuwa wanachama walikuwa na imani kubwa na mshindi wa kura za maoni kwani alifanya kazi kubwa ya kukijenga chama na sio huyo waliomuacha katika kura za maoni .
“Kinachoendelea sasa hivi ndani ya CHADEMA ni ufisadi mtupu,” alisema Bi. Gama akiongeza kuwa yeye binafsi alitoka CCM na kujiunga na Chadema kutokana na mapungufu yaliyokuwepo ndani ya CCM ila kinachoendelea kwa sasa ndani ya Chadema anajuta kuingia Chadema na hivyo ameamua kuhama chama hicho kumfuata mtu wao waliyemchagua popote atakakokwenda .
“ Mwenendo wa chadema kwa sasa ni wa ovyo zaidi kuliko chama chochote cha siasa hapa nchini tulikuwa tukishuhudia CCM watu wakikatwa ila leo ndani ya Chadema imekuwa ni kawaida kuona wale waliochaguliwa na wanachama kukatwa na watu wachache akiwemo mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Freeman Mbowe .....tumechoka tunahitaji kwenda kupata Demokrasia ya kweli ACT wazalendo sio ndani ya chadema”
Huku Bw Mapunda akidai kuwa siasa za ukabila zinaendelea kukitesa Chadema na kuwa suala hilo la ukabila na kuwakumbatia mafisadi ndilo ambalo linaendelea kukitafuna chama hicho pia siasa za ukanda na kukumbatia ufisadi imekuwa ni kawaida Chadema.
Hivyo alisema katika kuhakikisha wana Chadema wilaya ya Ludewa na kote nchini wanapinga siasa za ukanda na zile za kuwachukua watu wenye tuhuma za ufisadi kugombea ndani ya chama hicho ni lazima wanachadema kuungana kupinga hali hiyo kwa kuhama ndani ya chama hicho na kujiunga na ACT wazalendo.
Aliyekuwa mwenyekiti wa BAWACHA wilaya ya Ludewa Bi Mtenga alisema kuwa uonevu na rushwa vimechangia wanachama na wananchi kukosa imani kabisa na chama hicho na sasa badala ya kuwa chama cha wanyonge kimekuwa ni chama cha wenye pesa na mafisadi jambo ambalo wao kama wananchi wa chini hawapo tayari tena kukaa ndani ya Chadema.
Akimkaribisha mgombea ubunge huyo aliyekatwa ndani ya Chadema Bw Haule na wanachama zaidi ya 500 wa chadema , katibu wa ACT wazalendo wilaya ya Ludewa Bw Alfred Ulaya alisema kuwa pia alipata kuwa kiongozi ndani ya Chadema wilaya ya Ludewa ila alihama pamoja na viongozi wengine kutokana na siasa za chuki ndani ya chama hicho na hatua ya kukumbatia ufisadi.
Hivyo alisema wanachama hao hawajachelewa kujiengua na chadema na kujiunga na chama cha ACT wazalendo kwani ni chama chenye misingi bora na chama pekee chenye malengo sahihi ya kulikomboa Taifa na Chadema na pamoja na umoja wao wa vyama vinavyo unda katiba ya wananchi (UKAWA) ni CCM B hivyo lazima watanzania wapenda mabadiliko lazima kuchagua ACT wazalendo.
Katibu huyo alisema kwa wanachama wote ambao wamejiengua na Chadema na kujiunga na ACT wazalendo wakiwemo makatibu na wenyeviti wa kata zaidi ya 10 waliojiunga na ACT wazalendo na viongozi wengine watakuwemo ndani ya chama hicho na vyeo vyao kama walivyotoka Chadema.
Kwa upande wake mgombea huyo aliyeenguliwa kugombea ubunge mbali ya kushinda kura za maoni Bw Haule alisema kuwa kimsingi aliyeteuliwa kugombea nafasi hiyo alikuwa amewaandikia barua baadhi ya viongozi ngazi ya wilaya ya kuwaahidi kuwapa pesa ,kufungua duka la vifaa mbali mbali pamoja na kuwahonga pikipiki barua ambayo aliinasa na kuwaonyesha wanachama hao.
Pia alisema kimsingi baada ya kuenguliwa kugombea nafasi hiyo alitaka kukaa kimya kama aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema Dr Slaa ila akaona kukaa kimya bado si jibu na hivyo kuamua kujiunga na ACT wazalendo na kuweka uozo huo wazi.
Bw Haule alisema kuwa kwa sasa atahakikisha anazunguka jimbo nzima kufikisha kilio chake kwa wana Chadema na kupinga kwa nguvu zote wagombea wa udiwani na ubunge wa Chadema kupewa kura na kuwa kwa sasa uhai wa Chadema katika wilaya hiyo umekufa rasmi

Post a Comment Blogger

 
Top