0
Dar es Salaam. Wakati wa hali ya sintofahamu ikiwa imetawala uteuzi wa mgombea atakayeungwa mkono na vyama vinne vya upinzani, imebainika kuwa mzozo unaochelewesha suala hilo ni mgombea ambaye Chadema haijamuweka bayana.
Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye ambaye anapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa mbele ya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kada wa NCCR-Mageuzi, Dk George Kahangwa, lakini hadi sasa vyama hivyo bado vinasita kumtangaza mteule wake.
Profesa Lipumba alikuwa amewaahidi waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa mgombea ambaye ataungwa mkono na vyama hivyo vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD angetangazwa Julai 14, lakini siku hiyo hakuna aliyetangazwa.
Badala yake viongozi wa Chadema, NLD na NCCR ndio waliofika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam ambako Profesa Lipumba aliahidi kuwa ndiko jina la mgombea huyo lingetajwa, wakati viongozi wa CUF hawakuonekana na baadaye jioni wakasema kuwa walikuwa na kikao cha ndani ya chama cha kutafuta ufumbuzi wa mambo ambayo walikuwa hawajakubaliana.
Vyama hivyo vitatu vikaeleza baadaye kuwa jina hilo litatangazwa ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, lakini siku iliyofuata CUF ilisema suala la kuachia chama kingine jukumu la kusimamisha mgombea urais litawasilishwa  kwenye kikao cha Baraza Kuu la chama hicho ambacho kitafanyika Julai 25, jambo ambalo lilikubaliwa na vyama hivyo vitatu.
Matamko hayo yamefanya suala la mgombea urais wa Ukawa kugubikwa na giza nene, lakini kwa siku tatu Mwananchi imefuatilia na kubaini kuwa mgombea ambaye yuko na hajatajwa rasmi kwa vyama hivyo vinne ndiye anayechelewesha mchakato huo na amesababisha kuwapo na hatari ya umoja huo kuparaganyika.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vilivyoanza kufanyika takribani wiki mbili jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa licha ya viongozi wa vyama hivyo kumpata mgombea wao wa urais katika kikao cha Julai 14 mwaka huu, walikwama kumtangaza kutokana na CUF kutokuwapo kikaoni ikielezwa kuwa wanapinga maendeleo ya mchakato huo.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa msimamo huo wa CUF umetokana na utata ulioibuka katika kikao cha Ukawa cha Julai 11 na 14,  baada ya wagombea wawili kati ya watatu, kukubali mmoja wao agombee urais, lakini chama chake kikasema kuwa kinachotakiwa ni Ukawa kutangaza jina la chama kitakachotoa mgombea na si jina la mgombea.
Tayari Profesa Lipumba ameshachukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CUF, wakati Dk Kahangwa amechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, huku mchakato wa Chadema ukiwa haujaanza.
Habari hizo zinaeleza kuwa awali kulikuwa na mvutano mkali kati ya Profesa Lipumba na Dk Slaa na kwamba katika kikao cha Julai 11, Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF alikubali kumuachia Dk Slaa agombee urais kupitia Ukawa, lakini inaonekana hata ndani ya Chadema bado hawajaafikiana kuhusu jina la mgombea.
Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa jina la mgombea urais limeshapatikana na linasubiri muda muafaka.
“Tutamtangaza mgombea urais wa Ukawa ndani ya wiki moja kama tulivyosema awali,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana.

Post a Comment Blogger

 
Top