0

Uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chadema katika Jimbo la Bariadi umeahirishwa baada ya kubainika kwa matukio yanayoashiria vitendo vya rushwa.


Wakizungumza baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo, wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya walisema hawataki kuingiliwa na virusi vya rushwa ndani ya chama hicho, kwa kuwa hali hiyo italeta mpasuko na makundi.

Wajumbe hao wameutaka uongozi Chadema kuwa makini na wanachama mamluki wanaohama kutoka vyama vingine vya upinzani ili wasikivuruge.

“Hatua ya kuahirishwa kwa uchaguzi inaonyesha ni namna gani chama kilivyo makini ili wanaotoa rushwa wajifunze umakini huu na wananchi waelewe kuwa chama kinatetea wanyonge,” alisema Makula Saguda.

Hata hivyo, mjumbe mwingine, Masanja Lujani alipinga hatua hiyo akisema kuahirishwa uchaguzi ni ubadhilifu ambao haufai akisisitiza kuwa kama wamekamata mtu akiwa anagawa rushwa wangemtoa katika uchaguzi na wengine wakaendelea.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Emmanuel Mbise alisema uchaguzi huo umeahirishwa baada ya kukamata watu wakigawa rushwa kwa baadhi ya wagombea.

“Chadema kinaaminiwa na kinapendwa na watu kwa sababu hakikubaliani na rushwa, kwa mujibu wa katiba na mamlaka niliyopewa, nimeamua kuahirisha uchaguzi hadi utakapotangazwa tena kutokana na uchaguzi huu kutawaliwa na rushwa,” alisema Mbise.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Wilson Mshuda ambaye pia ni mgombea katika jimbo hilo alisema: “Hatuwezi kunyamaza kimya, hata katiba ya chama kuanzia ukurasa wa 86 inaongelea mgombea ambaye ataonekana kutoa rushwa kwa wajumbe kuwa atakuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro.”

Jimbo la Bariadi lina wagombea 12 ambao ni Godwin Simba, Mshuda, Masanja Madoshi, Seni Silanga, Manyangu Kulemwa, Zacharia Shigukulu, Maendeleo Makoye, Sweya Makungu, Sitta Mulomo, Wilson Limbu, Slivatus Masanja na Ntemi Ndamo

Post a Comment Blogger

 
Top