0

Dodoma. Kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kuwazuia wananchi kusafiri kwenda Dodoma hadi Mkutano Mkuu wa CCM utakapomalizika, imepingwa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa vijana wa chama hicho, Mtemi Yareld.

Juzi, Mulongo alinukuliwa na vyombo vya habari akiwaagiza polisi kuwazuia watu wanaotaka kusafiri kwenda Dodoma.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime ambaye aliwataka wananchi wasio na shughuli maalumu ya kufanya kutosafiri kwenda Dodoma katika kipindi chote cha mkutano huo.

Hata hivyo, Yareld alipinga uamuzi huo akisema unakwenda kinyume na Katiba ya nchi.

“Naviomba vyombo vya juu vya uamuzi kuingilia kati na kufuta kinachotakiwa kutekelezwa na polisi,” alisema.

Alisema Katiba inaeleza kila raia wa Tanzania ana haki ya kusafiri kwenda popote ndani ya nchi ilimradi havunji sheria.


“Nashangazwa na uamuzi wa kiongozi mkubwa kama huyu kuwazuia wananchi kusafiri kwenda Dodoma kwa sababu ya mkutano,” alisema.

Alisema haoni sababu ya kupitishwa kwa uamuzi huo, kwani wananchi wanahitaji kushuhudia mkutano huo, ambao mwaka huu unafanyika kwa staili ya pekee na aina yake.

Aliongeza: “Watu kutoka maeneo ya Mwanza, Ukerewe, Geita na mengine watasafiri na wengi wako katika maandalizi ya kuja kwenye mkutano huu, wasinyimwe fursa hiyo.”

Alisema kuwa atakuwa miongoni mwa makada wa chama watakaowapokea watu kutoka sehemu mbalimbali kuja mjini Dodoma kuanzia leo.

Leo Kamati ya Maadili na Usalama ya CCM inaanza shughuli ya kupitia taarifa za wagombea 38 wa nafasi ya urais kisha kuwasilisha taarifa zake kwenye Kamati Kuu inayotarajia kukutana kesho mjini hapa chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.

Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula alisema juzi mjini hapa kuwa chama kitatumia vigezo 13 katika kazi ya kuwachuja watangazania hao kabla ya kuendelea na hatua nyingine.


MWANANCHI

Post a Comment Blogger

 
Top