0

MABINGWA wa Tanzania Yanga na wale wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Azam FC wamejichimbia kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii itakayofanyika Agosti 22 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mbali na maandalizi kwa ajili ya mchezo huo, timu hizo pia zinajifua kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 22. Yanga wako jijini Mbeya, ambako wamejichimbia kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo huku Azam FC wenyewe wameanza kambi Zanzibar, ambako watacheza mechi kadhaa za kirafiki.
Mabingwa hao wa Tanzania Bara tayari wameanza kucheza mechi za kirafiki, ambapo wiki iliyopita waliikung’uta Kimondo kwa mabao 4-1 na Alhamisi wanatarajia kushuka tena dimbani kucheza na Silver Strikers.
Yanga itaendelea kujipima nguvu na kunoa makali yake wakati Jumamosi itakapoikaribisha Zesco ya Zambia katika mchezo mwingine wa kirafiki utakaofanyika kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hivi karibuni lilitangaza kuwa mapato yatakayopatikana katika mchezo huo wa Ngao ya Jamii yatatumika kuagiza kontena la vifaa vya michezo ikiwemo mipira ya saizi 3,4, bips na cones, ambavyo vitasambazwa mikoani.
Aidha, Azam FC wakiwa kambini katika visiwa vya marashi ya karafuu Zanzibar kesho wataanza kujipima nguvu kwa kucheza na KMKM, ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao kuelekea katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya vijana hao wa Jangwani.
Mbali na KMKM, Azam FC inatarajia kucheza na Mafunzo na JKU katika mechi zingine za kujipima nguvu ikiwa kambini Zanzibar. Msemaji wa klabu hiyo, Jaffar Idd alisema kikosi hicho kinaendelea kujifua kwenye uwanja wa Amaan asubuhi na jioni kwa ajili ya mchezo huo na ile ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Tulifika salama kwenye Hoteli ya Ocean View na wachezaji wote wanaendelea vizuri kwa program ya mazoezi ya asubuhi na jioni,”alisema. Alisema mchezaji ambaye alipata majeruhi katika michuano ya Kagame ni Salum Abubakari, ameanza mazoezi.
Idd alizungumzia wachezaji ambao walikuwa mapumziko kwao baada ya Kagame akiwemo Jean Mugiraneza na Didier Kavumbagu kuwa watawasili leo Zanzibar kuungana na wenzao. Aidha, Idd alisema kuwa wanampa pole mchezaji wao Allan Wanga aliyefiwa na mama yake mzazi juzi.
Wanga anatarajiwa kuungana na kikosi hicho cha Azam Jumapili ya wiki hii kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga. Alisema Kocha anatengeneza kikosi hicho upya kuhakikisha kinakuja na nguvu mpya ili kuwa na mwanzo mzuri wa kuifunga tena Yanga baada ya kuichapa kwa penalti 5-3 katika robo fainali ya Kombe la Kagame.
Ushindi huo wa Azam FC ni sawa na kulipa kisasi cha kufungwa na Yanga 2-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa mwaka 2012

Post a Comment Blogger

 
Top