0
Watu wengi hupenda kuwa na uhusiano wa kimapenzi ulio wazi mbele ya jamii. Kitaalamu hili ni jambo jema, lakini linahitaji umakini katika kulitekeleza


Tafiti za masuala ya mapenzi zinaonesha kuwa miongoni mwa mambo yanayowafurahisha wanawake wengi nyakati hizi ni utambulisho. Dk. Robin Baker mshauri na mwanasaikolojia nchini Uingereza anathibitisha hili kwenye uchunguzi wake.

“Kwa nini hujanipeleka kwenu? Mbona hutoki na mimi kwenye mapumziko yako na rafiki zako mwishoni mwa wiki? Jamani napenda twende wote klabu.” Hizi ni kauli za kiu ya utambulisho wa uhusiano kwenye jamii.

Nikiweka sawa mwenendo wa mada hii, nisiwatenge wanaume kwa mbali, kwani nao hutajwa kuwa ni hodari wa kutangaza uhusiano wao na wasichana hasa warembo au wenye nafasi fulani kwenye jamii, lengo likiwa ni kujisifu na kuuambia umma kuwa “mmiliki wa mali ni mimi.”

Kama nilivyotangulia kusema, hilo ni jambo jema, lakini swali linabaki kwenye swali nani ajuaye faida na hasara za uhusiano ulio wazi kwenye maisha ya mapenzi? Bila shaka akili yako msomaji inatafuta majibu!

Rejeo la Utafiti wa Taifa la Waingereza linaonyesha kuwa wanawake wanane kati ya kumi na wanaume sita kati ya kumi walikiri kuwa udanganyifu kwenye uhusiano wao wa kimapenzi.

Hoja inayozaliwa kwenye utafiti huo ni hii: “Kuna faida gani kumtambulisha mpenzi mdanganyifu kwenye jamii?” Labda kabla ya kwenda huko tupitie faida za uhusiano wa wazi ambazo ni:Kujenga uaminifu, kuthibitisha chaguo, kufungua ukurasa wa kujisahihisha, kujifunga kwenye ramani ya penzi la kweli.

Baada ya kutazama faida tusonge hatua moja mbele kutazama hasara ambazo nyingi zimeanishwa na Dk. Robin kuwa ni za kisaikolojia. Inaelezwa kutambulisha penzi la mdanganyifu ni sawa na kupanda mti wa uchungu pale penzi litakapovunjika.

Ifahamike kuwa kadiri idadi ya wanaofahamu uhusiano inapokuwa kubwa ndivyo maumivu ya kuachana yatakavyokuwa. Jaribu kufikiria mtu ambaye umemtambulisha kwa wazazi, ndugu na marafiki halafu anakusaliti utawaambiaje uliowajulisha?

Ni wazi litakuwa jambo gumu kuwaambia wote, hii ina maana utakuwa utajiona mnyonge kila siku, wakati mwingine si kwa ajili ya kusalitiwa kwako bali kwa sababu rafiki yako amekutumia meseji ya kukuuliza hali ya mwenzako. 

Nashauri wapenzi wasitambulishane haraka haraka bila kuchunguzana vinginevyo wakisalitiwa watapata ugonjwa wa moyo. Ni nafuu kuachana na mwanaume asiyejulikana kwa marafiki zako, kuliko uliyemtambulisha kwa mbwembwe kwa ndugu zako na kuonekana naye mtaani kila siku.

Post a Comment Blogger

 
Top