0
HATUA ya Fredy Mpendazowe na Mgana Msindai kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatokana na kuhangaikia maslahi binafsi, anaandika Dany Tibason.

Msindai, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida alijiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana kwa madai, ndani ya CCM hakuna demokrasia.

John Shibuda, Katibu Mkuu wa Chama cha ADA TADEA amesema, wakongwe hao katika siasa waliondoka CCM kwa madai ya kukerwa na chama hicho lakini cha kushangaza wamerejea kwa mbwembwe.

Shibuda amesema kwamba, wanasiasa hao ni wanafiki ndani ya siasa na kuwa “mnafiki hafi hadi ameumbuka.” Amedai hatua ya kurejea CCM imewaumbua.
“Waliishambulia CCM wakiwa kwenye majukwaa ya Chadema, leo wamerejea kule walikokuwa wakishambulia,” amesema Shibuda.

Amesema, Mpendazowe na Msindai wamekuwa wakiuaminisha umma kwamba CCM ni chama cha hovyo “iweje leo warejee kule kule kwa hovyo?

“Watu wazima kama hao ni wanafiki ndani ya siasa na wamekula matapishi yao. Hawawezi kuaminika tena katika jamii na katika ulingo wa siasa kwa kuwa, ni wanasiasa maslahi.
“Siyo wanasiasa bali wamevaa vazi la siasa huku uhalisia ukiwa ni wanasiasa maslahi. Hakukuwa na maana kutumia majukwaa kuitukana CCM na baadaye kurudi.

“Walipotoka CCM kwenda Chadema walitumia majukwaa kuishambulia CCM na sasa wamerudi CCM kwa kuishambulia Chadema.”

Shibuda amesema, umri wa wanasiasa hao ulitakiwa kutumiwa kuwajenga vijana kifikra juu ya kuwepo kwa siasa safi ambazo ni za ukombozi.

“Kwa umri wa Msindai na Mpendazowe walitakiwa kuwa shamba darasa na urithi wa mawazo kwa vijana chipukizi wa kisiasa.

“Tujikumbushe jinsi Mpendazoe alivyoweza kutunga kitabu ambacho kiliweza kuelezea mambo mengi, leo ni aibu kwa msomi huyo kuonesha udhaifu wa kisiasa na kujidhalilisha,” amesema Shibuda.

Pia ameishangaa CCM kwa kuwapokea wanasiasa wachafu na ambao wamekuwa wakikisema chama hicho vibaya hadharani.

“Kauli ya Rais John Magufuli kudai anataka usafi ndani ya chama ni unafiki, sidahi kama kuna kanisa ambalo linaweza kumpokea muumini ambaye aliyemkataa Yesu au msikiti ambao unaweza kumkaribisha muumini ambaye alimkataa Mtume.

“Je, muumini wa Dini ya Kiislamu anaweza kuitukana Qur’an na baadaye akaanza kuisifia? hilo jambo haliwezekani.”

Post a Comment Blogger

 
Top