Baraza Kuu la Uongozi la Chama  cha Wananchi (CUF) limemteua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa kamati  ya muda ya uongozi hadi utakapoitishwa mkutano mkuu maalumu mwingine  baada ya ule wa awali kuvunjika. 
Mtatiro amekubali uteuzi huo na kwamba hawezi kukwepa  majukumu hayo muhimu. 
Baraza hilo lililoketi katika kikao chake cha  dharura juzi Jumapili mjini Unguja, liliamua pia kusitisha uanachama wa  baadhi ya watendaji wake waandamizi, kutoa karipio kali na kuwafukuza  baadhi yao. 
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za makao makuu ya  chama hicho, Vuga kilihudhuriwa na wajumbe 47 kati ya 60 na kiliongozwa  na Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali. 
Akitangaza maazimio ya kikao  hicho jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui  alisema katika kutekeleza jukumu hilo, Mtatiro atasaidiana na Katani  Mohamed Katani na Severina Mwijage. 
“Maamuzi hayo ni kwa mujibu wa  katiba ya CUF kifungu Na.101 na 118, vinavyolipa mamlaka baraza  kutekeleza hatua hiyo.” 
Mazrui alisema baraza hilo lilimteua John  Bashange kukaimu nafsi ya naibu katibu mkuu wa CUF – Tanzania Bara na  Mbaralah Maharangande kukaimu nafasi ya naibu mkurugenzi wa habari,  uenezi na uhusiano kwa umma. 
Nafasi zilizojazwa ziliachwa wazi na  Profesa Ibrahim Lipumba, Magdalena Sakaya na Abdul Kambaya ambao baraza  hilo la dharura lilitangaza kuwasitisha uongozi na uanachama wao. 
“Hatua  ya kuitisha baraza la dharura sambamba na maamuzi hayo ilikuja baada ya  kushindwa kupata uongozi wa juu wa chama kufuatia kuvunjika na  kushindwa kukamilika kwa mkutano mkuu maalumu wa uchaguzi wa Agosti 21  uliofanyika jijini Dar es Salaam,” alisema. 
Alisema kuwa baraza liliamua  kusitisha uanachama wa Sakaya kwa kushindwa kutekeleza kifungu cha  katiba ya CUF, Na. 122 na kwamba licha ya barua aliyotumiwa kumtaka  ahudhurie kikao hicho, hakufika bila ya taarifa yoyote ya msingi. 
Mazrui  alisema katika baraza hilo, ilielezwa kuwa Sakaya alidai kuzuiliwa na  wazee wa CUF wa Dar es Salaam kwa madai kuwa hicho hakikuwa kikao  halali. 
Wengine ambao uanachama wao umesitishwa ni Ashura Mustafa,  Mohamed Mnyaa, Kapasha Kapasha, Haroub Shaim, Omar Masoud na Thomas  Malima. 
Baraza hilo la CUF lilitangaza kumfukuza uanachama wa chama  hicho, Shashu Lugeye, baada ya kumsikiliza na kutoridhishwa na maelezo  yake. 
Wanachama waliopewa karipio kali ni Rukia Kassim Mohamed na Othman Mohamed. 
“Chama  kimechukua maamuzi  haya kuonyesha dhamira ya dhati na matumaini ya  umma wa Watanzania kwamba CUF ndiyo pekee iliyobeba dhana ya  mabadiliko,” alisema Mazrui. 
Taarifa kutoka ndani ya Baraza hilo  ziliarifu sababu tatu za kuchukua hatua hiyo kuwa ni hasara ya Sh600  milioni kiliyoingia kwa mkutano uliovunjika; njama ovu zilizodaiwa  kutekelezwa na baadhi ya watendaji wao; na jaribio la kuchafua taswira  ya chama hicho. 
Mazrui alisema mkutano mkuu maalumu, kabla ya ule wa  kawaida wa mwaka 2018 kwa mujibu wa Katiba, utafanyika pale chama hicho  kitakapopata uwezo wa kifedha. 
Akiandika katika mtandao wake wa Facebok, Mtatiro alisema,  “Nimepokea majukumu niliyokabidhiwa na Baraza Kuu la chama changu.  Siwezi kuepuka majukumu haya muhimu kwa wakati huu ambapo chama  kinahitaji mchango wangu. Niko imara sana, natambua nimepewa majukumu  wakati gani na nianze na mguu upi kwenda mbele”
 
Post a Comment Blogger Facebook