Katika  hali isiyokuwa ya kawaida Prof Lipumba ameendelea Kung’ang’ania kiti  cha uenyekiti wa chama chake cha CUF na kusema kikao kilichokaa jana  visiwani Zanzibar na kufanya maamuzi ya kuwasimamisha uanachama,  hakikuwa halali na kilikuwa nje ya katiba ya CUF, sababu mojawapo ikiwa  ni kuwekwa kando kwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.
“Kikao  hicho  hakikuwa halali, haiwezekani Baraza Kuu linakaa halafu Naibu  Katibu Mkuu Bara hajui, wala hakujulishwa, na bado kuna wajumbe wengine  hawakuhusishwa” Alisema Prof Lipumba
Lipumba  aliongeza kuwa ni kweli alijiuzulu uenyekiti, lakini baadaye aliamua  kuandika barua kwa Katibu Mkuu ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na  sasa yeye ndiye Mwenyekiti halali wa chama hicho.
“Nilimuandikia  barua ya kurudi kwenye nafasi yangu, akasema anasubiri ushauri wa  kisheria, lakini hadi sasa hakuna kitu, hiyo inamaanisha kuwa sasa mimi  naendelea na nafasi yangu, na niko ngangari kama mwenyekiti” Alisema Prof Lipumba.
Aidha aliongeza kuwa alitaka kujieleza katika mkutano mkuu mbele ya wanachama, lakini mkutano ule ukavurugwa.
Kuhusu  kuwepo kwa tofauti kati yake na Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif  Sharif Hamad, Prof Lipumba amesema kuwa huenda kuna tofauti kwa kuwa  mara nyingi huwa hamuelewi jinsi anavyokiendesha chama bila kifuata  misingi ya kidemokrasia.
“Katibu  Mkuu anamdharau na hampi heshima yake Naibu Katibu Mkuu Bara, mara  nyingi huamua mambo yake bila kushirikisha viongozi wengine, halafu sasa  anataka kufukuza wanachama, huwezi kuwa na chama halafu ufukuze  wanachama, wanachama wanatafutwa duniani kote, halafu wewe unawafukuza,  hizo ni dalili za uongozi wa kiimla, kuongoza chama unapaswa kujali  demokrasia na siyo kuwa dikteta ndani ya chama” Amesema
Kuhusu  Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uongozi, Lipumba  amesema kuwa hatambui maamuzi hayo, na wala hamtambui Mtatiro kama  kiongozi wa chama hicho bali mjumbe wa Mkutano Mkuu, nafasi ambayo yeye  ndiye aliyempa.
“Mtatiro  hawezi kuwa mwenyekiti, mimi ndiye mwenyekiti wa chama, Mtatiro  alishindwa hata kuongoza mkutano mkuu, ukavurugika, hawezi, simtambui”

 
Post a Comment Blogger Facebook