0
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, utakuwa kati ya wagombea na makapi ya CCM na wananchi watachagua wagombea wa chama hicho tawala.
Akizungumza jana katika Ofisi Ndogo ya CCM Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam baada ya Mgombea Urais wa chama hicho, Dk John Magufuli kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kinana alisema kutokana na hilo, chama hicho kitashinda kwa kuwa na wagombea na sio makapi.
Katika siku za karibuni, Chadema, imewapokea wanachama wa CCM wanaohama kwa hasira baada ya kukosa uteuzi wa urais na ule wa ubunge.
Kati yao, yumo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Mahanga na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mgana Msindai.
Lowassa tayari alichukua fomu ya urais ya Chadema akiwa mgombea pekee na jana alipitishwa kuwa mgombea wao wa urais na pia chini ya mwamvuli wa Umoja wa vyama vinne vya upinzani vinavyounda Ukawa.
Kinana aliwaambia maelfu ya wanachama, mashabiki na wapenzi wa CCM waliojitokeza katika ofisi hiyo kumsindikiza Dk Magufuli kuwa: “Kwa bahati nzuri mwaka huu, tunashindana na makapi ya CCM. Uchaguzi Mkuu utakuwa kati ya wagombea na makapi ya CCM. Sasa kati ya makapi ya CCM na wagombea, mtachagua nani? (alijibiwa watachagua wagombea).
“Kila anayetemwa na CCM anakwenda wapi…(anajibiwa Chadema). Kwa hiyo hayo makapi hayatusumbui sisi. Sasa Ukawa imegeuka Ukiwa. Sasa wataisoma namba na namba yenyewe ni namba moja,” alitamba Kinana.

Post a Comment Blogger

 
Top