0
Kama mnavyojua ni kwamba, Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilikutana jana Mjini Zanzibar kujadili masuala kadhaa. Miongoni mwa hoja zilizozua mjadala mkubwa ni pamoja na Nafasi ya CUF ndani ya UKAWA. Katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi hakuhudhuria kwa sababu zilizoelezwa kuwa yupo nje ya nchi. Hata hivyo, taarifa za chini ni kwamba, Maalim alikwepa kuhudhuria kikao hicho kwa vile alijua nini Baraza litaamua.

Katika kujadili Mgombea Urais wa UKAWA, Wajumbe wengi wa kutoka Unguja na Tanzania Bara waliafiki Lipumba kuwa Mgombea Urais. Hata hivyo, wajumbe wanaotoka Pemba na baadhi ya wachache wa Bara walisisitiza kuwa CUF isiteue Mgombea Urais kwa madai kuwa chama hakina fedha za kampeni ya Urais.

Baada ya majadiliano ya Muda mrefu, hatimaye Baraza liliamua kwamba CUF wawe na msimamo wa kuhakikisha kuwa ni Prof. Lipumba ndiye atakayepeperusha bendera ya UKAWA kuwania Urais. Pamoja na hayo, Baraza limeshauri kuwa ikiwa kutakuwa na mazingira ya CHADEMA kulazimisha kuteua mgombea Urais, ufafanuzi wa masuala kadhaa utolewe na kuwashawishi viongozi wa CUF. Masuala hayo ni juu ya;

1.Mgawanyo sawa wa fedha za ruzuku baada ya uchaguzi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba fedha za ruzuku hutolewa kulingana na idadi ya wabunge. Hivyo, kama CHADEMA watasimamisha mgombea Urais, watakuwa na advantage ya kupata viti vingi vya wabunge na hivyo kupata kitita kikubwa cha fedha za Ruzuku. Baraza limeshauri kuwa kama CHADEMA wataridhia, fedha za ruzuku zigawanywe sawa baina ya vyama washirika wa UKAWA kwa vile wagombea ubunge watakaopatikana watapigiwa kura na wafuasi wa vyama vyote.

2.Mgawanyo sawa wa viti maalum vya wabunge. Baraza limeshauri kuwa CHADEMA watoe ufafanuzi wa jinsi watakavyogawana idadi ya wabunge wa viti maalum. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wabunge wa viti maalum hupatikana kutokana na idadi ya kura alizopata mgombea urais wa chama husika. Kutokana na Mgombea wa UKAWA kupigiwa kura na wafuasi wa vyama husika, Baraza la Uongozi linapendekeza mgawanyo sawa wa viti maalum vya wabunge vitakavyopatikana baina ya vyama vinavyounda UKAWA.

Bado haijafahamika ikiwa CHADEMA wataafiki masharti haya. Ikiwa wataridhia, ni dhahiri sasa CHADEMA wana nafasi ya kusimamisha mgombea Urais anayeandaliwa. Kama CHADEMA hawataafiki, Baraza limeshauri kuwa CUF wasimamishe mgombea wao ambaye ni Profesa Lipumba na watangaze rasmi kujitoa kwenye UKAWA.

Uongozi wa CUF utatoa taarifa rasmi kesho makao makuu ya chama Buguruni Dar es Salaam ingawa najua kuwa watapindisha pindisha kwa lengo la kunusuru UKAWA.

Post a Comment Blogger

 
Top