0
Nape: Wanaohama CCM ni sawa na mafuta machafuCHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uteuzi wa wagombea ubunge na uwakilishi, utazingatia yale yaliyofanyika katika uteuzi wa mgombea wao wa urais, na kusisitiza kuwa kuongoza kura za maoni sio mwisho wa safari, bali kigezo cha kuelekea katika uteuzi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, kama ilivyofanya katika uteuzi wa Urais ulimwibua Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, chama hicho hakitashindwa kusimamia maadili, taratibu na kanuni za uteuzi zilizowekwa na CCM katika kuteua wabunge na wawakilishi.
Nape aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam kuwa vikao vya uteuzi vitaanza Agosti 6, mwaka huu kwa Halmashauri Kuu Maalumu ya Taifa kukutana Zanzibar, na vitahitimishwa Agosti 12 na 13, wakati NEC itakapokutana mjini Dodoma.
“Kura za maoni za ubunge, uwakilishi, udiwani, ubunge wa Viti Maalumu zimekamilika kwa sehemu kubwa nchini. Yapo maeneo machache yanakamilisha kazi hiyo leo (jana). Lakini kazi hiyo kwa kiasi kikubwa imeenda vizuri na sasa vikao vya uteuzi vimeanza kwa ngazi za wilaya kwa udiwani wameanza leo (jana) kwa Kamati za Siasa za Wilaya kukutana,” alisema Nape na kuongeza:
“Kazi ya kuchuja kwa upande wa ubunge na uwakilishi itaanza Agosti 6 na 7 kwa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar kukutana na kufuatiwa na vikao vya Sekretarieti vitakavyokutana Agosti 8 na 9.”
Alisema Kamati Kuu itakutana Agosti 10 na 11, mwaka huu kabla ya NEC ya CCM kukutana kwa siku mbili kuanzia Agosti 12 na 13, ambayo inatarajiwa majina ya wagombea wa uwakilishi, ubunge na ubunge wa Viti Maalumu yaliyopitishwa na chama hicho yatawekwa hadharani.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi alisema uteuzi huo utazingatia mambo yote muhimu yaliyopewa vipaumbele katika uteuzi wa Mgombea wa Urais wa CCM, akisisitiza uadilifu na kutovunja kanuni za chama hicho.
“Kama ilivyokuwa katika uteuzi wa Mgombea wa Urais, uteuzi wa wabunge, wawakilishi na madiwani utazingatia mambo yale yaliyozingatiwa katika uteuzi huo. Watu watakaojihusisha na rushwa hawatakuwa na nafasi. Hilo limesimama.
“Hatuwezi kusimama barabarani na kuanza kuwasafisha watu na madodoki, muda huo hatuna, tuna muda wa kuwatafutia watu kura. Kama tumelifanya hili kwa wagombea urais, huku halitatushinda,” alisisitiza Nape ambaye ameongoza kura za maoni za ubunge Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Alisema kushinda au kuongoza kura za maoni sio mwisho wa safari, bali ni kigezo katika kuelekea kwenye uteuzi, huku wakiangalia kama mgombea anakubalika, lakini ikigundua upungufu katika mchakato uliowezesha ushindi wa mgombea, haitasita kuchukua hatua stahili ikiwamo kuchukua wagombea wa chini au kufuta matokeo yote.
“Huko nyuma tumewahi kuchukua hatua ikiwamo kuchukua mshindi wa pili au wa tatu na hata wa nne. Tumewahi kufuta kabisa matokeo yote ya jimbo zima, tumewahi kuwaondoa walioongoza. Imetokea Singida Mjini, Ulanga, Kigamboni,” alieleza Nape akitoa mifano ya NEC kuchukua hatua katika uteuzi baada ya kura za maoni.

Post a Comment Blogger

 
Top