0
WASOMI mbalimbali nchini wamewatahadharisha wananchi kwa kusema nchi haijafikia wakati wa wanasiasa kutaka kushinda uchaguzi kwa gharama yoyote, hata kama hawana misingi ya utawala bora.
Wakitoa maoni yao Dar es Salaam jana, wasomi hao kutoka taasisi za vyuo na zile za utafiti, walisema pamoja na kwamba kuhama chama ni haki ya mtu na hakuna anayeweza kuhoji, lakini wakahoji ni nini dhamira ya kuhama huko na kama kuna maslahi kwa wananchi.
Akizungumzia uamuzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutangaza kujiunga rasmi na Umoja wa Vyama Vinne vya Upinzani (Ukawa) na kukihama chama tawala, CCM, Mhadhiri Mwandamizi aliyebobea katika uchambuzi wa masuala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alihoji dhamira yake ni ipi.
“Kuhama chama ni haki ya raia, hakuna anayehoji, lakini dhamira inayompeleka Ukawa ni nini, hivi mtu aliyekuwa haramu kwao leo ni lulu, hapa ndio wasiwasi unaanza. Mwaka 2010 walimtumia Lowassa kama mtaji, mwaka 2015 wanamuona ni dhahabu, kuna uwalakini hapa”, alisema Dk Bana.
Alifafanua kwamba katika medani za siasa, haiwezekani mtu mmoja tena kwa ghafla anakuwa maarufu ndani ya vyama vinne na kusema huo ni unafiki uliokubuhu na hakuna demokrasia, kwani hata huko anakokwenda ataasi na kuwageuka.
“Lowassa anatoka CCM kimwili, na Ukawa walimdhalilisha sana Lowassa, walimnyanyasa na sasa ni vyema wakatubu hadharani kabla ya kupiga hatua nyingine yoyote, wamuombe awasamehe, na kwa vile Lowassa alishasema yeye ni Mkristo safi, basi awasamehe”, alisema Dk Bana.
Dk Bana akifafanua zaidi alisema haiwezekani taasisi hizo nne yaani vyama vya siasa vinne vinavyounda Ukawa, NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD, kukosa mtu wa kumsimamisha kwenye uchaguzi ujao hadi kusubiri CCM ikamkate jina Lowassa na ndio wao wakaona anafaa kupitia umoja wao.
“Tunapozungumzia masuala ya siasa tuangalie mbele zaidi, tujiulize hivi hawa viongozi wa vyama hivi vinne wana dhamira ya kweli kwa nchi hii, kinachoonekana hapa ni uroho wa madaraka na jambo hilo litafifisha vyama hivyo vyote kisiasa,” alionya Dk Bana.
Alisema haitakuwa ajabu ifikapo siku ya uchaguzi, watanzania sio mbumbumbu wataamua, hawawezi kuvutwa na mtu mmoja tu, bali wataangalia dhamira zao na maslahi ya taifa.
Alihadharisha kwamba jambo hilo la Lowassa kuondoka CCM litambomoa kisiasa na kamwe haliwezi kuijenga Ukawa kwani inavyoonesha kila mmoja ana dhamira yake binafsi na kwamba hakuna maadili wala sheria inayotumika kuongoza safari hiyo ya Ukawa.
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa masuala ya Uchumi kutoka REPOA, Dk Abel Kinyondo alisema Ukawa wamemtumia Lowassa kama chambo cha kuvuta watu wengi, jambo ambalo alisema ni mbinu moja ya kushinda uchaguzi.
Lakini akaonya kuwa, siasa ni zaidi ya kushinda uchaguzi, na kusema ni vyema Ukawa wakatafakari uamuzi wao kwani jambo hilo linauweka umoja huo njia panda. “Kwa kumpata Lowassa wanaweza kushinda uchaguzi, lakini je, maadili na sheria, Ukawa inasimamia wapi?
Vyama vinatakiwa kuwa na maadili na msimamo vilete sera nzuri kwa wananchi sasa, miaka mitatu mfululizo walimsema Lowassa mchafu, na anatakiwa awe amefungwa, sasa wamemsafisha lini hadi awe msafi kusimama Ukawa? Alihoji Dk Kinyondo.
Alisema, Tanzania haijafika kipindi cha wagombea kushinda kwa gharama yoyote, bali inahitaji viongozi wasafi na wanaoweza kutetea maslahi ya wananchi, na sio wenye nia na maslahi binafsi ya kung’ang’ania madaraka kwa nguvu.
“Ni vyema tungeambiwa Ukawa wanasimamia wapi, walishatoa matamko sio, Dk Slaa wala Mbowe ya kuwa Lowassa ni fisadi na anatakiwa afungwe, sasa leo amegeuka kuwa msafi kiasi gani hadi wamsimamishe kuwakilisha vyama hivyo vilivyomtuhumu? Alihoji Dk Kinyondo.
Katika hilo, Dk Kinyondo alisema uamuzi wao huo, utawaacha njia panda na utashusha hadhi ya vyama hivyo kwani kama wanashindwa kusimamia misimamo yao miaka chini ya mitatu tu, wakiwa nje ya madaraka, je, wakiingia watawezaje kuongoza kwa utawala bora na kuhadharisha wananchi wanatakiwa kuwa macho.
“Siasa ni zaidi ya kushinda uchaguzi, ni kuangalia maendeleo ya watu yatakuwaje na misingi ya utawala bora ni ipi na misimamo ya chama au vyama ni ipi katika kuongoza nchi,” alisema Dk Kinyondo.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bashiru Ally, alisema hadi sasa hakuna mwanasiasa yeyote aliyehamia chama kingine cha siasa, kutokana na kuendeshwa na itikadi ila wengi wanahama kutokana na maslahi yao binafsi.
“Hata hivyo, kuhama huku hakujaanza leo, katika historia ya vyama vingi tumeona wanasiasa wengi tu wakubwa, wakihama vyama vyao kwenda vyama vingine hasa ikifikia nyakati za uchaguzi na sababu kubwa ni malengo ya kisiasa,” alisema.
Alisema wengi wa wanasiasa hao huhama kutokana na njaa ya kutawala hivyo wanapokosa fursa walikotoka huhamia kwingine kuitafuta fursa hiyo. “Huu si mwenendo mzuri kwani unaonesha kuwa wanasiasa wengi hawafuati kanuni za vyama vyao bali malengo yao binafsi,” alihtimisha.
Amkimbia Lowassa Katika hatua nyingine, kada wa Chadema, Innocent Peter Kamani akizungumza kupitia kipindi cha Hello Tanzania kinachorushwa na kituo cha Redio cha Uhuru FM jijini Dar es Salaam, alitangaza kurudisha kadi ya Chadema na kuwa mwanaharakati kutokana na chama hicho kumpokea Lowassa, akisema kimehadaa wanachama wake, kwani kwa muda mrefu walikuwa wakimsema kwa mabaya mwanachama mpya waliyempokea, hivyo kuwayumbisha wanachama kuhusu msimamo halisi wa chama hicho.

Post a Comment Blogger

 
Top