0
Hai. Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe amesema kampeni za mwaka huu zitakazofanywa na umoja huo, hazijawahi kuonekana tangu nchi ipate uhuru 1961.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, alisema Ukawa itafanya kampeni kwa kutumia usafiri wa anga na ardhini na kuongeza kuwa safari hii hakutakuwa na mgombea wa CCM atakayesimama bila kupingwa na upinzani.
Ukawa unaundwa na vyama vinne ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF) na vyote vimekubaliana kuweka mgombea mmoja wa urais, ubunge na udiwani.
Hata hivyo, hadi sasa umoja huo haujamtangaza atakayewania urais na pia haujaweka wazi majimbo ambayo wamekubaliana kuachiana ili kusimamisha mgombea mmoja.
“Tutafanya kampeni, ambazo hazijawahi kuonekana nchini. Naomba mtembee kifua mbele kwa sababu nina hakika tunakwenda kuchukua dola kutokana na kampeni za kisayansi tutakazokwenda kufanya,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe alitoa kauli hiyo juzi wilayani Hai, wakati akiwashukuru wanachama wa Chadema waliomchagua baada ya kupata kura 269 kati ya kura 274 zilizopigwa katika Jimbo la  Hai.
Mbowe aliionya CCM kutotarajia mteremko na hata zile jitihada zao za kutaka kushinda uchaguzi kwa goli la mkono hazitakubalika.
“Tunaiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya kazi kwa weledi ili uchaguzi uwe wa huru na haki,” alisema na kuongeza:
Mwenyekiti huyo aliwataka wanachama wanaounda Ukawa na wafuasi wake kujiandaa kwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini wa Chadema, Mchungaji Israel Natse alisema hawakichukii chama tawala, bali matendo mabaya kama ufisadi na rushwa yanayofanywa na viongozi wake.

Post a Comment Blogger

 
Top